Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waandishi Kilimanjaro wafunga ofisi yao wakidai kuwepo ubadhirifu

Baadhi ya Waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro wakiweka kufuli kwenye ofisi za Klabu ya wanahabari Mkoani humo (Mecki).Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro, wamelazimika kufunga ofisi za Klabu ya Wanahabari mkoani humo (Mecki) kwa madai ya matumizi mabaya ya ofisi pamoja na kutosomewa mapato na matumizi.

Moshi. Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro, wamelazimika kufunga ofisi za klabu ya waandishi wa habari mkoani humo (Mecki) kwa madai ya matumizi mabaya ya ofisi pamoja na kutosomewa mapato na matumizi.

 Ofisi hiyo imefungwa Juni 5 na wanahabari hao kwa kile walichodai kuwa Mei 12, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya siku ya vyombo vya habari duniani yaliyofanyika mkoani humo walitoa siku 21 za kikatiba kwa klabu hiyo kutoa taarifa ya mapato na matumizi jambo ambalo halijafanyika kinyume na maagizo hayo.

Hata hivyo, waandishi hao ambao ni wanachama na wasio wanachama walifika katika ofisi hiyo wakiwa wamebeba makufuli ambao walimkuta mratibu wa chama hicho aliyekuwepo ndani ya ofisi hiyo na kumwomba kutoka nje ili waweze kufunga ofisi hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti waandishi hao walisema lengo la wao kufunga ofisi ni kuutaka uongozi wa klabu hiyo kutekeleza maagizo waliyopewa Mei 12, mwaka huu.

Dixon Busagaga mwandishi na mwanachama wa klabu hiyo, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kushindwa kufikia makubaliano yaliyotokana na kikao cha siku ya habari, kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa bodi ya Kahawa.

"Tuliafikiana na uongozi kutoa taarifa ya zile hoja zetu zilizoibuliwa wakati wa kikao baada ya siku 21 ...Miongoni mwa hoja hizo ni kwa nini mkutano mkuu haujafanyika tangu mwaka 2019, pili taarifa ya mapato na matumizi na hapa tulitaka taarifa ya fedha kutoka benki, haya yote yanaonekana kukwama," alisema Busagaga.

"Tumefanya hatua hii kama sehemu ya kupaza sauti kwa walezi wetu ambao ni Umoja wa vilabu vya wanahabari Tanzania (UTPC) kuja kuweka suluhu ya mgogoro huu ambao umeanza kujitokeza," amesema. 

Naye Gift Mongi, ambaye ni mwandishi wa habari mkoani humo, amesema viongozi hao wa Klabu wamekuwa wakikwepa majukumu yao na hawatekelezi yale ambayo ni ya kuwasaidia waandishi mkoani humo.

Mongi ameeleza kuwa zipo mali za chama zilizotolewa na wadau ikiwemo Pikipiki iliyotolewa na Hayati Philemon Ndesamburo ila hakuna mapato na matumizi ya pikipiki hiyo huku kukosa hakuna Uwaziri katika taarifa za viongozi wa Klabu hiyo.

"Mali hiyo ilitolewa kwa waandishi wa habari wa Kilimanjaro na siyo kwa wanachama pekee ila ukiuliza viongozi wanadai kuwa hupaswi kuuliza kama siyo Mwanachama hata katiba ya Mecki haisemi hivyo maana tulipewa kama Waandishi wa habari wa Kilimanjaro, viongozi hawapo wazi katika mambo yao," amesema.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Bahati Mustapha amesema kuwa hajapata taarifa hizo.

"Kwa sasa sijapata hizo taarifa naomba niwasiliane na viongozi wengine wa klabu ya wanahabari kufahamu zaidi," amesema Bahati.