Wabunge EAC walia corona kuathiri shughuli zao, waendelea na mikutano kwa mtandao

Muktasari:

Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wasema ugonjwa wa corona umeathiri shughuli za utendaji wao, pamoja na wafanyabiashara

Dar es Salaam. Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), tawi la Tanzania wamesema mlipuko wa maambukizi ya ugonjwa wa corona umeathiri shughuli zao za utendaji wakisema hadi hivi sasa bado wanaendesha vikao vyao kwa njia ya mtandao.

Mbali na hilo, wamesema ugonjwa huo umeathiri shughuli za wafanyabiashara wa jumuiya ambao baadhi yao wameshindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana hali hiyo.

Hata hivyo, wamesema kunahitajika suluhuhisho la kudumu la namna ya kukabiliana na ugonjwa huo ndani ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo badala ya kutegemea chanjo kutoka mataifa ya Ulaya.

Wabunge hao walieleza hayo leo, Ijumaa Machi 5, 2021 wakati wakizungumza na wanahabari kuhusu umuhimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zilizopo.

Mwenyekiti wa wabunge hao tawi la Tanzania, Adam Kimbisa amesema ugonjwa wa corona umeathiri wao kukutana na wenzao kutoka nchi jumuiya katika vikao badala yake shughuli hiyo inafanyika kwa njia ya mtandao.

"Umeathiri sana na walioathirika ni wafanyabiashara ambao wanakaa muda mrefu mpakani kutokana taratibu za kukabiliana na ugonjwa zilizowekwa na nchi wanachama wa jumuiya.

"Hakuna wa kumlaumu kwa sababu kila nchi imejiwekea utaratibu wake wa kukabiliana na ugonjwa huu. Kilichopo ni kuilaani hii Covid-19 tu," amesema Kimbisa.

Akizungumzia kuhusu uwepo wa jumuiya hiyo, Kimbisa amesema umesaidia  kuwa umoja wa forodha  ulioanza rasmi mwaka 2005 ukilenga kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi wanachama kufuatana na kanuni za uasili wa bidhaa.

"Imesaidia kuwa na wigo mmoja wa ushuru wa bidhaa zinazotoka nje ya jumuiya, kuanzisha kwa himaya moja ya forodha. Kuanzishwa kwa vituo vya pamoja vya utoaji wa huduma mipakani," amesema Kimbisa.