Wabunge Tabora wamwangukia Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi mkoani Tabora

Muktasari:

Wabunge wanaotoka katika majimbo ya Mkoa wa Tabora wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa majimbo yao.

Tabora. Wabunge wanaotoka katika majimbo ya Mkoa wa Tabora wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa majimbo yao.

Wabunge hao wametoa rai hiyo leo Alhamisi Mei 19, 2022 wakati wa ziara ya Rais Samia ambayo anaifanya mkoani humo.

Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka amemuomba Mkuu huyo wa nchi kuingilia kati mgogoro wa mipaka katika jimbo hilo kati ya wananchi na maeneo ya majeshi.

Amesema wananchi wamekuwa wakisumbuliwa na hata walioondolewa wametolewa pasipo kulipwa fidia.

"Tunaomba wewe ukiwa kama Amiri Jeshi Mkuu uingilie kati suala hili" amesema.

Akizungumzia ushuru wa mazao, amesema sasa wananchi wanatozwa hata debe moja la mahindi badala ya kuanza kutozwa kuanzia tani moja kama alivyoagiza aliyekuwa Rais John Magufuli.

Amesema mgambo wamekuwa wakiwasumbua wananchi na kutaka tamko lake kuhusu hali hiyo kama limeondolewa au la.

Mbunge wa Viti Maalum, Munde Tambwe amemweleza Rais kuwa wajawazito bado wanatakiwa kutoa fedha wanaponda kujifungua na vifaa havionekani vya kujifungulia na kutaka hali hiyo irekebishwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Tabora, Magreth Sitta amedai simu yake kujaa malalamiko ya wakulima wa tumbaku kuhusu kutolipwa madai yao baada ya kuuza tumbaku.

Amesema kuna changamoto kubwa katika zao la tumbaku kwa vile wakulima wengi bado hawajalipwa malipo ya tumbaku yao waliyouza.

Ametaka changamoto ya wakulima wa tumbaku kushughulikiwa ili wanufaike na kilimo hicho.

Magreth ameomba Tabora kupewa chuo kikuu kutokana na kuwa kitovu cha elimu

Amesema aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliahidi Ujenzi wa Chuo Kikuu mwaka 2015 na kuomba Rais Samia alichukue lifanyiwe kazi.

Naye Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali amedai kuwa Mkurugenzi wa halmashauri yake amekataa kutoa fedha za miradi ya maendeleo alizoomba Sh100 milioni kutoka katika halmashauri.

Amesema kuwa alipata fedha Sh500 milioni kutoka kwa wafdhili kwaajili ya miradi ya maendeleo lakini ilitakiwa Sh100 milioni zitoke halashauri kuunga mkono fedha hizo alizozitafuta kwa wafadhili ambapo amedai kuwa mkurugenzi alikataa kutoa.

Amesema kuwa pamoja na kufikisha suala hilo kwa mkuu wa mkoa, amesema limeshindwa kushughulikiwa.

"Mheshimiwa Rais mimi kazi yangu kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo lakini mkurugenzi amegoma kutoa fedha " amesema.

Mbunge huyo ameeleza kuwa hata alipotaka fedha hizo kutoka mfuko wa maendeleo ya Jimbo, bado mkurugenzi alikataa.

Rasi Samia yupo uwanja wa Mwinyi katika ziara yake ya siku tatu, leo ikiwa siku yake ya mwisho.