Wabunge Tanzania watakiwa kupaza sauti kupinga rushwa, uzembe

Wabunge Tanzania watakiwa kupaza sauti kupinga rushwa, uzembe

Muktasari:

  • Wabunge na watumishi wa Bunge 39, kati ya hao wabunge wakiwa 21, wamemaliza mafunzo ya mwezi mmoja ya kwa mujibu wa sheria ambayo yametolewa na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) na kutakiwa kupinga rushwa, uzembe na utumiaji wa dawa za kulevya kwa vijana.

Dodoma. Wabunge na watumishi wa Bunge la Tanzania wametakiwa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupaza sauti zao katika kupinga uzembe, rushwa na utumiaji wa dawa za kulevya kwa vijana.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Agosti 5,2022 na Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Nchini (JWTZ), Meja Jenerali Paul Simuli wakati wa kufunga mafunzo kwa mujibu wa sheria kwa kundi maalum la wabunge na watumishi wa Bunge yaliyotolewa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 834 Makutopora, Dodoma.

 “Ninawasihi sana ndugu zangu wabunge, tukapige kelele kwa kuwaelimisha Watanzania mambo haya wayaache ili tuweze kumuunga mkono mheshimiwa Rais na nchi yetu iweze kusonga mbele,” amesema.

Pia Meja Jenerali Simuli amewataka wabunge hao kumuunga mkono Rais Samia katika dhana ya viwanda kwa kulipigia kelele jambo hilo ili vijana wa Kitanzania wapate ajira katika sekta hiyo.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa JKT, Kanali Erasmus Bwegoge amesema wana imani baada ya kuhitumu mafunzo hayo, watatekeleza majukumu yao kwa weledi, uzalendo na uharaka mkubwa ili kuongeza tija katika maendeleo ya Taifa.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Makutopora JKT, Luteni Kanali Festo Mbanga amesema ni imani yao baada ya mafunzio hayo wataonyesha mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kiuwajibikaji ndani ya Bunge, majimboni mwao na kwa Taifa kwa ujumla.

“Mafunzo haya yamewajengea uzalendo, nidhamu nzuri, ari ya kuchapa kazi bila kuchoka, umoja na mshikamano ndani yao na uvumilivu wanapopambana na changamoto mbalimbali katika maisha yao. Ni matumaini yetu makubwa wataleta mabadiliko makubwa ndani ya Bunge letu,” amesema Luteni Kanali Mbanga.

Naye Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi amesema mafunzo hayo yameongeza mabalozi wa JKT bungeni na kuwa tija ya mafunzo hayo itaonekana katika muhimili huo.

Akisoma risala ya wahitimu hao, Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msavatambangu amesema kutokana na manufaa ya mafunzo hayo hasa katika suala la uaminifu, utii, uhodari, wepesi katika maamuzi na uzalendo wanapendekeza wateule wa Rais kuwekewa utaratibu wa mafunzo hayo.

Ametoa mfano wa wateule hao ni wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wakuu wa idara kwa kuweka utaratibu wa kupitia mafunzo hayo kwa muda utakaoonekana kuwa unafaa kabla ya kuanza kufanya kazi walizoteuliwa kuzifanya.

Amependekeza pia somo la uzalendo kufundishwa kwa umakini kama mada mahususi kwa wanafunzi ngazi zote za elimu kuanzia msingi hadi vyuo vikuu.