Wabunge wa CCM kulivalia njuga sakata la GN 28 Mbarali

Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa (NEC) Ndele  Mwaselela akimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Mbarali kwa tiketi ya chama hicho, Bahati Ndingo (katikati) kushoto ni mwenyekiti wa CCM wilayani Mbarali. Picha Marry Mbwilo

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa tangazo hilo wananchi wanatakiwa kupisha maeneo hayo ili maji yatiririke vema katika mto Ruaha na Bonde la Ihefu ili kutunza mazingira na kusaidia shughuli za uzalishaji wa umeme.

Mbarali. Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaoshiriki kampeni za ubunge wa jimbo Mbarali, mkoani Mbeya; wamejiapiza kulipigia kelele suala tangazo la gazeti la Serikali namba 28 la 2008 (GN28), linalowazuia wasifanye shughuli za maendeleo ya kudumu kwenye baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa tangazo hilo wananchi wanatakiwa kupisha maeneo hayo ili maji yatiririke vema katika mto Ruaha na Bonde la Ihefu ili kutunza mazingira na kusaidia shughuli za uzalishaji wa umeme.

Wabunge hao wakiongozwa na Livingstone Lusinde (Mvumi), walitoa ahadi hiyo jana Alhamisi Septemba 14, 2023 kwenye kampeni za kuwania ubunge ambapo walimuombea kura Bahati Ndingo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ubaruku.

Uchaguzi wa mdogo wa Mbarali unatarajia kufanyika Septemba 19 mwaka huu kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Francis Mtega, ambaye aligongwa na trekta dogo (Power Tiller) shambani kwake.

Wamesema wanatambua umuhimu wa ardhi katika shughuli za uzalishaji mali kikiwemo kilimo ndiyo maana wanabeba jukumu la kuishawishi Serikali ilitazame kwa kina tangazo lake la mwaka 2008 ili kuwapa unafuu wa maisha wananchi.

Lusinde amewataka wabunge wenzake kubeba suala la tangazo hilo la Serikali kwa lengo la kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu utakaowezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.

"Twendeni tukamsaidie huyu (Bahati), sio suala la kucheka, hawa wananchi wana shida, hawalimi nasema kwa uchungu hili Mama Mary Chatanda upo hapa leo, upo na makamu wako Zainab na mjumbe wa Kamati Kuu nyie ni watu wakubwa kweli tushindwe GN?” amehoji mbunge huyo na kuongeza;

"Haiwezekani twendeni kwa umoja wetu, tukazungumze na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa tumeshinda Mbarali lakini ahadi yetu ondoa hii (GN), kweli tutashindwa? Naomba Wana Mbarali mpeni kura Bahati," amesema Kibajaji na kuibua shangwe kwa wananchi wa Ubaruku Mbarali.

Hata hivyo, Septemba 10 wakati akizindua kampeni za kuwania kiti hicho, Ndingo alimpa ujumbe Rais Samia kupitia Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda akimtaka mkuu huyo wa nchi kuruhusu wakulima kulima maeneo yaliyozuiliwa wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Katika hotuba yake, Lusinde maarufu kama Kibajaji alisema endapo Ndingo akifanikiwa kupata ushindi wa jimbo hilo atamshangaa ikitokea akaunga mkono bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii pasipo GN 28 kubadilishwa, akimtaka kukaa kwa kuwa wananchi wa Mbarali kwa sababu CCM kuna demokrasia.


Leo Ijumaa akiwa katika kijiji cha Magigiwe Ndingo aliwaomba wananchi wa wamchague ili akatatue changamoto zao mbalimbali ikiwemo ya GN 28 kwa shirikiana na wabunge wenzake wa chama hicho tawala akisisitiza yeye ni mtu sahihi wa kuongoza jimbo hilo.

Mkazi wa Magigiwe Fahad Said alimuomba Bahati kuweka mkazo zaidi katika sekta ya michezo, akisema vijana wa Mbarali wanapenda michezo lakini hawawezeshwi hivyo akishinda atupie jicho suala hilo.

Katika mkutano huo mgeni rasmi alikuwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM  (UWT), Mary Chatanda aliyeambatana na Makamu wake, Zainabu Shomary, Katibu wa NEC na Oganaizesheni Issa Ussi Gavu, Mbunge wa Makete, Festo Sanga, Mbunge wa Makambako, Deo Sanga, na Mbunge Viti Maalumu Khadija Shaaban 'Keisha'.