Wabunge waitaka Serikali itwae maeneo jirani na Bunge

Muktasari:

  • Wabunge wametaka Serikali kutwaa maeneo yanayozunguka Bunge ili kupata nafasi ya kujenga ofisi za wabunge na kuimarisha usalama.

Dodoma. Wabunge wametaka Serikali kutwaa maeneo yanayozunguka Bunge ili kupata nafasi ya kujenga ofisi za wabunge na kuimarisha usalama.

Hoja hiyo imetolewa leo Mei 26 na Joseph Mhagama (Madaba-CCM), Halima Mdee (Viti Maalum) na Cosato Chumi (Mafinga Mjini-CCM).

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa 2022/2023 Mhagama amesema kuwa kwa mazingira yaliyopo, viongozi na umuhimu wa muhimili wanahitaji ulinzi na usalama wa hali ya juu.

“Lakini leo ili wabunge wako waweze kushiriki katika mazoezi na kulitumikia taifa vizuri inawabidi kwenda nje ya eneo hili wanakodi viwanja maeneo mbalimbali ya mji,”amesema.

Amesema upo ushahidi mwingi unaonyesha kuwa eneo hilo halitoshi kwa shughuli za kibunge ikiwemo wabunge kukosa ofisi.

“Hata wananchi wangu wa madaba wakija nakutana nao kantini nilihitaji nikae nao katika maeneo ambayo ninaweza kuongea nao masuala ya maendeleo,” amesema.

Amesema mambo yatakayofanya bunge kufanya kazi zake vizuri ni kuwa na mazingira rafiki, salama itakayofanya wabunge wafanye kazi kwa ufanisi mkubwa.

Amesema anajua jitihada zilizofanywa na Bunge ikiwemo kufanya tathimini ya majengo na viwanja lakini aliomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ichukue jukumu hilo ili kuwa na Bunge la kisasa linaloweza kutoa huduma bora.

Amesema anafahamu kuwa wapo katika hatua za mwisho za kupitisha bajeti inaweza kuitisha kamati ya Bunge ya Bajeti ikafanya marekebisho.

Kwa upande wake Halima amesema kuwa hoja hiyo ilishapelekwa katika Wizara hiyo kwa hiyo ni vyema ikatoa maelezo ili kama kuna hoja ya kufanyiwa kazi basi ifanyiwe kwa haraka.

“Kwasababu siku hazigandi na dhamani ya ardhi inapanda kila siku, kwa hiyo ni lazima uamuzi ufanyike haraka kwa maslahi ya Bunge lakini na wananchi kwa ujumla,” amesema.

Naye Chumi amesema kukosekana kwa ofisi kumefanya wabunge kukaa na wananchi wao nje ya eneo la Bunge kwenye maegesho ya magari ili kuzungumza nao na kuomba Serikali kulifanyia kazi kwa haraka jambo.