Wabunge wataka ukomo upelelezi

Muktasari:

  • Wabunge wametaka Serikali kuweka ukomo wa upelelezi na kutekelezwa kwa sharti la kisheria la kuzuia kukamatwa kwa mtuhumiwa kabla ya upelelezi kukamilika.


Dodoma. Wabunge wametaka Serikali kuweka ukomo wa upelelezi na kutekelezwa kwa sharti la kisheria la kuzuia kukamatwa kwa mtuhumiwa kabla ya upelelezi kukamilika.

Wabunge hao ni Mbunge wa Lupembe Edwin Swale na Neema Lugangira (Viti Maalum) ambao wamesema hayo walipokuwa wakiuliza maswali ya nyongeza bungeni leo Ijumaa Septemba 23, 2022.

“Watu wengi wanakaa sana mahabusu na kesi zao zinachelewa ni lini Serikali italeta marekebisho ya sheria kuweka ukomo kwa makosa ya jinai.

“Kwa kuwa makosa mengi watu wanakaa mahabusu hayana dhamana ni lini Serikali italeta sheria kuruhusu makosa yote kuwa na dhamana.” Ameuliza Swale

Akijibu kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwan Kikwete amesema sheria inayohusiana na upelelezi ilipelekwa bungeni kwa ajili ya marekebisho.

Amesema marekebisho hayo madogo yalifanyika ya kuruhusu upelelezi kufanyika kabla ya kesi kupelekwa mahakamani.

“Serikali chini ya Rais imeendelea kufanya marekebisho ili kukidhi haki jinai,”amesema Kikwete.

Naye Neema amesema mwaka jana bunge lilibadilisha sheria ya ukamataji kabla ya kukamilisha upelelezi lakini jambo hilo bado halitekelezeki na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan amelisemea na kutolea maelekezo.

“Serikali haioni umuhimu wa kufanyia marekebisho Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ili kuweka ukomo wa upelelezi kama Zanzibar walivyofanya.

“Serikali haioni haja ya kuweka masharti nafuu ya dhamana kwa watu ambao hawana mali kwa sababu hivi sasa masharti ya dhamana ni makubwa kuliko makosa kana kwamba wanakomoa wananchi” amehoji

Akijibu swali hilo Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, George Simbachawene amesema Katiba na sheria ziko wazi katika mfumo wa haki wanaotenda jinai na wanatendewa jinai.

Amesema hivi karibuni kulikuwa na tatizo la panya road nchini lakini inavyosemwa bungeni ni kwamba polisi wasikamate watuhumiwa hao hadi upelelezi.

Amesema waliotendewa makosa ndio wanaotakiwa kuhurumiwa zaidi ya wale waliotenda makosa ya jinai.

Simbachawene amesema kwa kufanya hivyo ndio maana nchi iko salama hadi hivi sasa.