Wachimbaji madini kuchangamkia fursa Chunya

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon Mayeka.

What you need to know:

  • Wachimbaji waeleza ya moyoni kuelekea maonesho ya kwanza ya teknolojia ya Madini na fursa za uwekezaji Mkoa wa Mbeya yanaotarajia kufanyika Mkoa wa kimadini Chunya.

Chunya. Kwa mara ya kwanza Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya itakuwa na maonyesho ya teknolojia ya madini na fursa za uwekezaji Mkoa wa Mbeya yanaotarajia kuanzia Machi 14 hadi Marchi 18, 2023 wachimba wa madini ya dhahabu wamesema hiyo ni fursa kwao katika kukuza uchumi ili kuhamasisha uchimbaji madini na kuona vifaa vya kisasa.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon Mayeka amesema hayo alipozungumza na madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri wilayani hapa ambapo amewataka wachimbaji wa madini ya dhahabu wajitokeze kuona vifaa vya kisasa vitakavyoletwa kwenye maonesho hayo.

Mayeka amesema Wilaya ya Chunya kwa masuala ya madini inajulikana kama mkoa wa kimadini Chunya na kwamba itafanya maonyesho ya teknolojia ya madini na fursa za uwekezaji Mkoa wa Mbeya ambapo amedai maonesho hayo yataongeza uzalishaji na kubainisha kuwa kwasasa Wilaya inazalisha kilo 300 za dhahabu kila mwezi.

Wakizungumzia Maonyesho hayo yatafanyika viwanja vya Sinjilili, Kata ya Itewe wilayani baadhi ya wachimbaji wamesema hiyo ni fursa kwao ya kuona teknolojia ya kisasa katika uchimbaji na uchenjuaji madini ya dhahabu.

Mchimbaji wa madini kutoka Mtaa wa Itumbi aliyejitambulisha kwa jina la Idd Maganga  amesema wachimbaji watatembelea maonesho hayo ili kupata ujuzi kwenye matumizi ya vifaa vya kisasa vya kuchimbia.

"Wachimbaji wengi wilayani Chunya wamebadilika ukilinganisha na zamani kwani siku hizi wanatumia mitambo kama skaveta kuchimbia badala ya sululu na chepeo, hata hivyo bado wanahitaji ujuzi zaidi ili kuchimba dhahabu bila kubahatisha,’’ amesema.

Mchimbaji mwingine Ollu Keneth amesema wanahitaji teknolojia itakayowasaidia kuondokana na kuchimba kwa mkono kwenye mashimo yao ambayo mazingira yao ni hatari.

Naye mchimbaji Willfred Aron amebainisha kuwa maonesho hayo yatasaidia kuongeza ufanisi katika uchimbaji na kuondoka na ajali zisizo za lazima.

Aidha Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka akizungumzia maonyesho hayo, amesisitiza wananchi kushiriki kwa wingi ili waweze kujifunza kwenye sekta ya madini ya dhahabu na kuboresha kazi zao ili kuongeza uzalishaji.

"Naomba wachimbaji na wananchi wote waweze kushiririki kikamilifu kwenye maonesho ya kwanza ya teknolojia ya madini inayotarajia kufanyika kwa siku nne katika mkoa wetu wa kimadini Chunya ili kujifunza mbinu mpya ili zitakazowasaidia katika kazi zao na kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha," amesema Mbunge Kasaka.