Wachumi waugusa mradi wa Dege Village
Dar es Salaam. Tamko la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) la kupata mnunuzi wa mradi wa Dege Village uliokwama kwa miaka saba, limeibua maoni tofauti ya wadau wa uchumi.
Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari alisema taratibu za umaliziaji wa zabuni ya uuzaji wa mradi kwa mteja ambaye hakuwekwa wazi, zitakamilika Oktoba 31, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mshomba, mradi huo utauzwa kwa Sh501 bilioni, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa bodi ya NSSF na Serikali, ili kurudisha fedha za wanachama zilizowekwa kwenye mradi huo.
Hatua hiyo imewaibua wadau wa uchumi, wakisema Serikali ilipaswa kuutekeleza mradi huo kusaidia kupunguza mrundikano wa nyumba za makazi eneo moja mkoani Dar es Salaam na wengine wakisema uamuzi huo ni sahihi kwa sababu unaepusha hasara zaidi ambayo ingeweza kutokea.
Profesa Enock Wiketye, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Uchumi, akizungumza na Mwananchi jana, alisema anaunga mkono hatua ya uuzaji wa mradi huo kutokana na kutotengeneza faida.
Alisema uamuzi huo ulipaswa kuchukuliwa mapema kwa sababu fedha zilizotumika zilikuwa za wanachama na si za NSSF.
“Kama mradi umeshindwa kukamilika ina maana waliotakiwa kunufaika ambao ni wanachama wa NSSF hawawezi kunufaika tena na NSSF yenyewe inataka fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine, bila kuuza mradi huo hauwezi kuzipata,” alisema.
Tafsiri nyingine aliyoitoa profesa huyo wa uchumi juu ya mradi huo kuuzwa, ni NSSF kutumia nia hiyo kama suluhu ya kukabiliana na upungufu uliobainika wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Profesa Wiketye alisisitiza kuwa mradi wa Dege Village hadi kuuzwa, umekwenda kinyume na mategemeo ya NSSF.
Hata hivyo, Profesa Abdallah Safari alisema kilichochangia mradi huo kuuzwa ni matatizo ya kisera. “Hayati Rais John Magufuli alipoingia madarakani alisema hataki masuala ya nyumba bali viwanda, kulikuwa na mradi wa nyumba za Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) Kawe ulisimamishwa, kwa hiyo kuuzwa kwa huu mradi ni hasara kubwa sana, mimi nilitamani uendelezwe na Serikali,” alisema Profesa Safari.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Greyson Mgonja, akisema: “Jukumu la kuuza ni kutaka kurejesha fedha, kusudi NSSF itekeleze miradi mingine iliyosimama kutokana na kukosekana kwa fedha, japo kwangu naona huu ni uzembe, hupaswi kuuza mradi ili uziingize kwenye miradi mingine.”
Pia, alihoji kama wote waliotafuna fedha za mradi huo waliwajibishwa, huku akisema kama bado, kuendelea kuwaacha ofisini ni kufungua mianya ya kuteketea kwa miradi mingine.
Gladnes Munuo, aliyejitambulisha kuwa ni mwananchi wa kawaida, alisema hatua ya NSSF kutekelea mradi huo ililenga kusaidia wananchi kupata makazi bora.
Hata hivyo, alishauri mnunuzi aliyepatikana naye atembee katika mawazo ya NSSF ya kusaidia sekta ya makazi nchini.
Kwa upande wake, Maulid Kikondo, mchambuzi wa masuala ya kiuchumi alisema uuzwaji wa mradi huo unatokana na kupoteza mwelekeo ambao ulitarajiwa.
“Ukisema uundeshe mradi wakati huna mtaji maana yake utakuwa unafanya nje ya mtaji, kwa hiyo suluhu ni kuuza kwa mwenye mtaji ili aweze kumalizia ili mradi utekelezwa na uanze kuingiza pesa, kwa hiyo haya maamuzi yana faida japo si ya moja kwa moja, lakini huwezi kuukumbatia mradi ambao tayari umefeli,” alisema Kikondo.
Mradi huo ambao mpaka kukamilika kwake ungekuwa na thamani ya Sh1.3 trilioni, NSSF iliingia katika ubia na Azimio Housing Estate Limited (AHEL). Katika ubia huu NSSF inamiliki asilimia 45 na AHEL asilimia 55. Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni thamani ya ardhi.
Mwaka 2016 NSSF walitoa mradi huo wenye nyumba 3,750 kwa Kampuni ya Yono ili kuunadi na fedha waliyotarajia kupata ni Dola350 milioni za Marekani, sawa na Sh811.7 bilioni, lakini mnunuzi hakupatikana.
Hadi mradi huo unauzwa ukiwa umeshatumia Sh330 bilioni ukiwa kwenye eneo la ekari 302 wilayani Kigamboni.
Ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2014 na kusimama mwaka 2016, ulidaiwa kutumia zaidi ya Sh179 bilioni, hivyo kutokamilika kwa nyumba za kifahari, hoteli, maduka makubwa eneo la mapumziko, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa kungekuwa na hasara kubwa.