Wadau KIA watakiwa kushiriki vita dhidi ya ugaidi

Kamanda wa Polisi wa viwanja vya ndege nchini Jeremiah Shilla Akizungumza na wasafirishaji uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) picha Mussa Juma.

Muktasari:

  • Wasafirishaji wa abiria na mizigo, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA),wametakiwa kushiriki kudhibiti  kutokea matukio ya uhalifu.

Arusha. Wasafirishaji wa abiria na mizigo, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wametakiwa kushiriki kudhibiti matukio ya uhalifu, ikiwapo ugaidi katika uwanja huo.

Kamanda wa viwanja vya ndege nchini,Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jeremiah Shilla  ametoa agizo hilo leo Desemba 5,2022 wakati akizungumza na wasafirishaji wa abiria na mizigo, katika uwanja huo,.

Shilla amesema wasafirishaji hao wanawajibu mkubwa   kushiriki vita dhidi ya uhalifu kwani KIA ikiwa salama nao wataendelea kunufaika.

“leo nimekuja hapa kuwapongeza kwa ushirikiano wenu mzuri na polisi kituo cha KIA hadi kufanikiwa kukamatwa baadhi ya watuhumiwa  ,nawataka muendee kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwani KIA ikiwa shwari na nyie mtaendelea kunufaika”amesema

Amesema uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ni eneo muhimu kwa taifa kwani ndio lango  kuu la watalii wanaokuja nchini, hivyo maadui hupenda kufanya uhalifu katika maeneo kama hayo.

Awali mkuu wa kituo cha polisi cha KIA, Edith Makweli amesema ushirikiano mzuri baina ya polisi na wasafirishaji KIA umewezesha kukamatwa watuhumiwa kadhaa katika siku za karibuni.

Makweli amesema watuhumiwa hao, baadhi walifika uwanja wa bodaboda na gari lakini kabla ya kufanikisha mipango yao, taarifa tulipata na tukafatilia hadi kuwakamata wengine walikuwa tayari wakikimbilia nchi jirani.

Wasafirishaji Uwanja wa KIA

“Kwa sasa tunaendelea kuimarisha ulinzi lakini pia tunaimarisha polisi jamii katika vijiji na vitongoji vyote kuzunguka uwanja huu wa KIA”amesema

Diwani wa kata ya KIA,Tehera Kipara ameeleza kuridhishwa na ushirikiano ambao wamekuwa wakipata kutoka kituo cha polisi KIA na hadi  kupunguza matukio ya uhalifu.