Wadau wa habari walia na Sheria ya Uhalifu Mtandaoni

Muktasari:
Imeelezwa kuwa Sheria ya Uhalifu Mtandaoni ina maneno yanayoweza kumuathiri mwandishi wa habari kwa kiwango kikubwa.
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa Sheria ya Uhalifu Mtandaoni ina maneno yanayoweza kumuathiri mwandishi wa habari kwa kiwango kikubwa.
Hayo yameelezwa leo Jumatano jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA – TAN), James Marenga alipokuwa akizungumza kwenye semina na wanahabari kuhusu sheria mbalimbali zinazohusu taaluma ya habari.
Ametaja baadhi ya maneno yenye mitego katika sheria hiyo kuwa ni pamoja na yale yanayotamka ‘kwa namna nyingine’ au ‘kusudio na kinyume cha sheria’. “maneno kama ‘kwa namna nyingine au kusudio na kinyume cha sheria,’ ni hatari yanayotumika kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria. Maneno haya unaweza kuyaona kuwa ya kawaida, lakini ni hatari,” amesema Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea.
Wakili Marenga amesema, katika sheria hiyo kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema Kifungu cha 7 (i)(g) cha sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2015, kimevuruga uhuru wa faragha akisema taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.
“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) inaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila mhusika kuwepo.
“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini na kwa kosa gani. Ndio maana tunasema sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,” amesema.
Akiunga mkono upungufu uliopo katika sheria hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema baadhi ya vipengele vinapaswa kuondolewa kabisa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile
‘’Sheria inaruhusu kesi yako kuendeshwa bila wewe mwenywe kujua. Kesi unaweza kufunguliwa Mwanza, siku unapita mitaani unakuta unapigwa tanganyikajeki. Ndio, wanaweza kufanya hivyo, sheria inaruhusu. Tunapopigania hii sheria iondolewe au ipitiwe upya, watu wajue tunapigania masilahi ya wengi,’’ amesema Balile.