Wadau wa habari wamshukia Dk Abbas, wadai hakumuelewa Rais Samia

Wednesday April 07 2021
hassanpic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Wakati Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas akidai Rais Samia Suluhu Hassan alivyotamka vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe hakumaanisha magazeti yaliyofungiwa, wadau  mbalimbali wamemshukia kwamba hakuielewa kauli ya kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Dk Abbas alitoa kauli hiyo jana Jumanne Aprili 6, 2021 wakati akihojiwa na televisheni ya Wasafi saa chache baada ya  Samia kuagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa kufunguliwa katika hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“...,lakini ni kusimamia vyombo vyetu vya habari ndani, nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia fungia sijui vi televisheni vya mkononi  vifungilieni lakini wafuate sheria na miongozo ya serikali. Tusiwape mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa vyombo vya habari lakini mhakikishe kila mliyempa ruhusa ya kuendesha chombo cha habari anafuata sheria za serikali na kanuni ziwe wazi kosa hili adhabu yake hii..., tusifungie tu kibabe tuhakikishe wanafuata kanuni,” alisema Samia.

Wakati wadau wakimshukia Dk Abbas, jana taarifa ya kurugenzi ya mawasiliano ya rais Ikulu ilieleza kuwa kiongozi mkuu huyo wa nchi ameagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe na kutakiwa kuzingatia sheria.

Katika mahojiano hayo, Dk Abbas alisema agizo hilo liligusa vyombo vya habari vya mtandaoni pekee na kwamba magazeti hayahusiki akisisitiza kuwa iwapo rais ataagiza magazeti yaliyofungiwa yafunguliwe watalifanyia kazi hilo.

“Rais alizungumzia kuhusu vyombo vya habari vya mtandaoni na unafahamu kuwa amefanya mageuzi kule TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) kwa hiyo tutakwenda kuangalia ni vyombo vipi vilifungiwa na kutokana na sababu zipi kisha tutachukua hatua kama alivyoelekeza Rais.”

Advertisement

“..., kwa hiyo tutalifanyia kazi hilo lakini kama kuna maelekezo mengine sisi ni watekelezaji tunatekeleza. Rais amesisitiza vyombo vya habari kuendelea kuzingatia maadili na sheria za nchi lakini kwa hili agizo alilolitoa tunakwenda kuchukua hatua mara moja,” amesema.

Muda mfupi  baada ya kauli hiyo wadau hao walitumia mitandao ya kijamii ya Twitter na Instagram kumshukia Dk Abbas wakidai kuwa katibu mkuu huyo ndio hakuelewa alichokieleza Samia.

Katibu mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema, “uamuzi wa Dk Hassan Abbas kulipa tafsiri finyu agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufunguliwa kwa vyombo vya habari akidai hajaagizwa kufungulia magazeti ni online Tvs tu ni dalili kuwa kichwani kwake bado anaishi zama za...,”

“Katika muktadha ambao Rais Samia alikuwa anazungumzia uhuru wa vyombo vya habari Dk Abbas alipaswa kuchukulia Online Tv kuwa ni mfano tu wa vyombo vingi vya habari vilivyofungiwa.”

Deodatus Balile ambaye pia ni mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ameandika, “Dk Hassan Abbas sijakusikia vizuri. Unasema Rais hakuagiza mfungulie Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima?”

“Isikilize tena hotuba ya mama au unataka kuwa wa kwanza kuzinguana, Asante sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia kuagiza vyombo vya habari vifunguliwe.”

Katibu wa jukwaa hilo, Neville Meena amesema Dk Abbas bado ana hamu ya kuendelea kufungia magazeti kwa kutafsiri maelekezo ya Rais Samia.

“Eti amri yake inahusu kufunguliwa kwa online tv tu, ndugu yetu huyu hajifunzi,” amesisitiza Meena.

Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema amesema, “ni kweli uhuru wa vyombo vya habari ni haki yetu na sio kwa hisani ya watawala, lakini pia dhamira ya mtu sio haki yetu. Hivyo tunapoona dalili za dhamira njema kwa mtu ni vyema tukatambua kwa sauti kuu kwani roho nzuri Tanzania imekuwa bidhaa adimu kati ya mwaka 2015 hadi 2020.”

Advertisement