Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wa haki jinai wabainisha tishio la uhalifu wa mtandao

Muktasari:

  • Jumla ya washiriki 60 kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika na mfumo wa haki jinai wanahudhuria mafunzo maalumu kuhusiana na tatizo la uhalifu wa kimtandao huku wadau wakionesha unavyogharimu matrilioni ya fedha duniani, Afrika.

Dar es Salaam. Wadau wa haki jinai kutoka taasisi mbalimbali nchini Tanzania wamenolewa kwa kupewa mafunzo ya namna ya kukabiliana na tatizo la uhalifu wa kimtandao huku wawezeshaji wa mafunzo wakibainisha hali ya uhalifu huo ilivyo nchini na duniani.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika jijini Dar es Salaam, yamefunguliwa leo Jumatano, Septemba 2, 2024 na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuia ya Madola kwa ufadhili wa Serikali ya Uingireza.

Mkuu wa Utawala wa Sheria wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, Dk Elizabeth Macharia, amesema Afrika inapoteza Dola za Marekani milioni 4 ambazo ni karibu na asilimia 10 ya pato lake, kwa mwaka kutokana na uhalifu wa kimtandao.

Macharia amesema duniani gharama za uhalifu wa kimtandao zinatarajiwa kufikia Dola 23.84 trilioni kufikia mwaka 2027 kutoka Dola za Marekani 8.44 trilioni mwaka 2022.

Akifungua mafunzo hayo, Jaji Mwarija amesema mafunzo hayo yanaakisi juhudi za Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola katika kupunguza kiwango na athari za uhalifu wa mitandaoni katika nchi za Jumuiya ya Madola.

Jaji Mwarija amesema uhalifu wa kimtandao unaleta changamoto ambayo inaendelea kukua kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia na kwamba mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kubadilishana maarifa, uzoefu, na namna bora ya ushughulikiaji makosa hayo.

Amesema mafunzo hayo yataimarisha maarifa na ujuzi wa majaji, waendesha mashtaka na wapelelezi kuhusiana na maendeleo ya hivi karibuni katika sheria za uhalifu wa kimtandao na namna ya kushughulikia ushahidi wa kielektroniki.

Pia, amesema watapanua uelewa wao wa sheria zinazosimamia makosa ya uhalifu wa kimtandao na kujadili changamoto wanazokabiliana nazo katika upelelezi, kuendesha mashtaka na kuamua kesi hizo.

Jaji Mwarija amesema ukusanyaji, uhifadhi na upokewaji wa ushahidi wa kielektroniki ni mambo muhimu kuhakikisha mafanikio katika kuendesha kesi na uamuzi wa haki.

“Kama mlinzi wa haki, mahakama ina jukumu la msingi kuhakikisha kuwa kesi za uhalifu wa kimtandao zinaamuriwa kwa haki na kwa ufanisi wakati ikizingatia utawala wa sheria na kulinda haki za binadamu,” amesema Jaji Mwarija.

Jaji Mwarija amesema wapelelezi wana jukumu la kukusanya na kuchanganua na kuhifadhi ushahidi na waendesha mashtaka wana jukumu la kuhakikisha kuwa wahalifu wa kimtandao wanafikishwa mbele ya sheria.

Hivyo amesema wanapaswa kuwa ufahamu sheria za makosa ya kimtandao na uwezo wa kuwasilisha ushahidi tata wa kielektroniki wa kwa namna inayoeleweka kwa mahakama.

“Kwa kufanya kazi kwa karibu na wapelelezi, waendesha mashtaka wanafanya jukumu la msingi katika kuhakikisha kuwa kesi za uhalifu wa kimtandao zinaendeshwa kwa ufanisi na kwa haki,” amesema Jaji Mwarija.

Kwa upande wake, Naibu Balozi wa Uingereza Nchini, Sally Hedley amesema kuwa kuwa tatizo la uhalifu wa kimtandao halina mipaka na kwmaba ni tatizo kubwa linalohitaji unyumbulifu kutoka vyombo vya utekelezaji sheria vya ndani kikanda na kimataifa.

“Uzoefu wetu binafsi nchini Uingereza unaonesha kwamba tishio linalosababishwa na uhalifu wa kimtandao linaendelea kukua na kuleta changamoto mpya za kiusalama”, amesema Hedley.

Akizungumzia tatizo hilo katika mataifa ya Afrika, amesema taarifa za Shirika la Polisi wa Kimataifa Interpol) zinaonesha linaendelea kukua kwa asilimia 25 kila mwaka na kwamba hakuna taasisi au mtu binafsi aliye salama.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kilichoandaa mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Paul Kihwelo amesema mafunzo yanawashikirikisha majaji 15 akiwemo mmoja kutoka Mahakama ya Zanzibar.

Amewataja washiriki wengine ni manaibu wasajili wanne, mahakimu wakazi wa mkoa 10, mahakimu wakazi wa wilaya watano na mahakimu wengine wa kawaida, wapelelezi sana na waendesha mashtaka wanane kutoka mikoa mbalimbali.

“Tumewaleta hawa wote watatu (wapelelezi, waendesha mashtaka na majaji na mahakaimu) ili wewe na uelewa wa pamoja wa namna ya kushughulikia makosa ya namna hiyo”, amesema Jaji Kihwelo na kuongeza:

“Na hi inatokana na kwamba sasa hivi uhalifu kwa kiasi kikubwa zaidi unafanyika katika mtandao kuliko uhalifu unaofanyika kwa njia ya kawaida.”

Akitoa mfano wa uhalifu wa wizi wa fedha duniani na bila kutoa takwimu, Jaji Kihwelo amedokeza kuwa kwa duniani fedha zinazoibiwa kwa njia ya mtandao ni nyingi zaidi kuliko kiasi cha fedha zinazoibiwa kwa njia za kawaida.

Amesema mbali na wawezeshaji wawili wa ndani, wawezeshaji wengi wa mafunzo hayo wametoka nchi za nje kama Uingereza, Dubai na nchi nyingine za Jumuiya ya Madola ambao watachambua sheria zilizopo nchini tayari.

Wakizungumzia mafunzo hayo, washiriki wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Mwandamiz, Ellen Masululi na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa, Honorious wamesema kuwa mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi na maarifa katika kutekeleza majukumu yao.

Wakili Masululi mafunzo hayo yatawasaidia katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yao kama vile kuamua kama kesi ifunguliwe au isifunguliwe baada ya kusoma majalada ya upelelezi kutoka polisi na uendeshaji mashauri mahakamani.

“Kwa hiyo sasa ufahamu huo tutakaoupata kupitia semina hii, utatusaidia kujua kama ushahidi nilionao wa makosa ya kimtandao na ushahidi wa Kielektroniki unatosha kwenda mahakamani au la,” amesema Masululi na kuongeza:

“Lakini pia yatawasaidia kuongoza upelelezi kwani sisi mawakili wa Serikali tuna nafasi ya kuongoza wapelelezi na kuwashauri namna ya kufanya katika kesi husika na tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa ushauri kuishauri ofisi.”

Hakimu Kando amesema kuwa anatarajia kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kutoa kuamua kesi wanazokumbana nazo hasa katika kipindi hiki ambacho kuna uhalifu mwingi wa kimtandao na makosa mengi yamekuwa yakifanyika kwa njia ya mitandao.

Amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko ya sheria ambapo kwa Sasa ushahidi wa kielektroniki unapokewa mahakamani na kwamba kwa kukizingatia kwamba makosa haya ni mapya na Sheria pia ni mpya, mafunzo hayo sasa yatawajengea uwezo namna kuamua kesi bila kukosea hasa.

Amesema kuwa uzoefu unaonesha makosa ya mtandao yanatokea ni mengi na sheria bado ni mpya na ufahamu bado ni mdogo kwa watu wengi na kwamba baada ya mafunzo hayo watakuwa wamejengewa uwezo wa pamoja.

“Tunategemea wapelelezi watapeleleza kesi zao vizuri kwa mujibu wa Sheria na itamrahisishia pia mwendesha mashtaka kuendesha kesi yake vizuri mahakamani na tunategemea Mahakama itatenda haki kwa mujibu wa mnyororo mzima wa haki jinai Kwa maana ya upelelezi, uendeshaji mashtaka na uamuzi,” amesema.