Wadau wabainisha vichocheo vya rushwa kwa trafiki
Muktasari:
- Taboa, Darcoboa wafunguka, polisi waeleza mikakati kukabili rushwa barabarani
Dar es Salaam. Masilahi duni na kukosekana uweledi kwa askari wa usalama barabarani, vimetajwa kuwa vichocheo vya kuwapo vitendo vya rushwa.
Hata hivyo, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) na Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), wameeleza si trafiki pekee wanaopokea rushwa, huku madereva na wamiliki wa mabasi wenye makosa barabarani wakitajwa kujihusisha na vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Agosti 7, 2024 na wadau waliochangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi X Space (zamani twitter) ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ukiwa na mada inayohoji, ‘Vitendo vya rushwa kati ya madereva na askari wa usalama barabarani, nini chanzo na nini kifanyike kuvidhibiti?
“Mshahara wa askari japo wana marupurupu haukutani na mshahara mwingine, hii inasababisha ukiachana na mfumo mzima wa maisha yao, askari hawa ni watumishi wa Serikali ambao tunategemea mtu aliyeajiriwa awe na mzigo mkubwa mabegani mwake, kusaidia familia yake na kuwa na mategemeo ya kustaafu vyema,” amesema mchambuzi wa masuala ya kijamii, Dk Faraja Kristomus.
Amesema mahitaji hayo makubwa na mshahara mdogo ndiyo huwachochea askari kupokea rushwa.
Mbali na hilo, amesema rushwa barabarani kati ya madereva na askari wa usalama barabarani ni ya ushirikiano.
Amesema mtoa rushwa hutekeleza kitendo hicho baada ya kutambua adhabu yake, hivyo hutoa kima cha Sh5,000 kukwepa kulipa Sh30,000.
“Anayepokea rushwa ya Sh5,000 anaona kama hiyo ni baraka kwake, uzoefu wa kijamii unaonyesha rushwa kwa Jeshi la Polisi ipo kwa ngazi zote, kuna baadhi ya watu wanadiriki kusema waziwazi kwamba ndani ya Jeshi la Polisi hakuna msafi kuanzia askari wa usalama barabarani, askari wa upelelezi wa kesi, wale waliopo ngazi za juu mikoani wananyooshewa vidole kwenye rushwa,” amesema.
Kutokana na kutokuwapo taasisi ya kulishughulikia Jeshi la Polisi, amesema wamekuwa wakilindana hivyo anayekemea rushwa ndani ya Jeshi hilo, Jeshi lenyewe humshangaa.
Dk Christomus amesema suala la rushwa lipo ndani ya mfumo mzima wa Jeshi la Polisi, hivyo huitajika taasisi madhubuti ya kushughulikia changamoto hiyo.
Akichangia mjadala huo, Elias Komanya amesema masilahi duni ndiyo sababu ya askari kupokea rushwa.
“Askari anaajiriwa akiwa peke yake, hana mke lakini hadi anapata familia mshahara huohuo haujawahi kupanda hivyo anaona bora atafute njia mbadala ya kupata pesa ili atunze familia yake,” amesema.
Amesema Serikali ifanye tafiti ikigundua rushwa ipo, itengeneze mazingira mazuri ya kazi ndipo ianze kuwasimamia.
Ukosefu wa uweledi
Mtaalamu wa Sheria, Clay Mwaifani amesema ili kudhibiti rushwa ni lazima kuwapo uweledi kwa vyombo vyote vinavyosimamia sheria.
Amesema takwimu mbalimbali zinaonyesha taasisi zenye dhamana ya kupambana na rushwa kama vile Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndiyo zinaongoza kwa rushwa.
“Mageuzi makubwa kwa Jeshi la Polisi na haki jinai ndiyo mbadala wa hii shida tunayoizungumza, lakini pia mitazamo ndani ya Serikali hakuna misimamo mikali juu ya rushwa,” amesema.
Clay amesema licha ya watu wakati mwingine kuona rushwa inatolewa kwenye vyombo vya usafiri walivyopanda, wanaogopa kukemea ili wasionekane viherehere wa kuharibu dili za watu.
Amesema kwa mujibu wa sheria, mtu yeyote ana mamlaka kisheria ya kumkamata mtu anayetoa rushwa.
Amesema masilahi duni na makazi mabovu ya askari ni kichocheo kwao kutumbukia kwenye lindi la kupokea rushwa.
Taboa, Darcoboa
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus John amedai rushwa barabarani kwa wakaguzi wote wa magari ni ya kiwango cha kutisha.
Amesema wanaopokea wanaonekana kuwa ni Jeshi la Polisi pekee kwa sababu wanavaa nguo nyeupe lakini ipo kwa wakaguzi wote.
Uwepo wa rushwa kati ya madereva na askari barabarani amesema unachochewa na tabia, mazingira na wamiliki wa mabasi na madereva kutofuata sheria, mazingira ya kazi kuwa magumu na watu kutoridhika na mishahara yao.
“Jambo la kufanyika ni rushwa kupigwa marufuku kuanzia shule za msingi, hata watu wazima sasa nao wapewe elimu ya rushwa namna inavyorudisha nyuma maendeleo kwa sababu unampa mtu haki isiyo yake, unamnyima mwenye haki. Rushwa Tanzania ni changamoto, hakuna sehemu ambayo haichukuliwi,” amesema.
Amesema barabarani yapo mageti mengi na magari yanakaguliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Ameshauri matumizi ya teknolojia katika ukaguzi wa magari akisema yatasaidia kubaini upungufu uliopo.
Amewataka wamiliki wa mabasi kutoingiza magari mabovu barabarani kuepuka mazingira ya rushwa.
“Tunatakiwa wamiliki na madereva kujitambua, hizi hela ndogondogo na biashara ilivyo ngumu tunaacha hela nyingi barabarani,” amesema.
Pia, ameshauri mazingira ya kazi ya Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani yaboreshwe ili kupunguza vitendo vya rushwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk amesema baadhi ya madereva na wamiliki wa mabasi wenye makosa barabarani ndio huwashawishi askari kuchukua rushwa ili wasiandikiwe faini.
Amesema kama gari lililopo barabarani halina tatizo lolote, hakuna sababu ya mtu kuogopa kusimamishwa na askari barabarani.
Amesema dereva, mmiliki wa mabasi au daladala akifuata sheria zote za usalama barabarani ni ngumu askari kumdai rushwa.
“Umevaa sare, hukatishi ruti, umepita njia yako kwa nini askari akusimamishe akudai rushwa, tusitake kumsingizia askari wakati dereva akiwa na makosa anatengeneza mazingira ya kumshawishi askari apokee rushwa,” amesema.
Utendaji wa Jeshi la Polisi
Mwandishi Mwandamizi wa Mwananchi, Elias Msuya alipochokoza mada hiyo amesema, “rushwa iko katika sekta nyingi inaanzia hata kwa waandishi wa habari, hospitali, mahakamani, watumishi wa umma, sekta binafsi. Kwa upande wa barabarani rushwa inaonekana waziwazi.”
“Wakati tunaandika habari ya rushwa tulibaini kwamba muundo wa Jeshi la Polisi kukosa udhibiti kwa maana makosa yapo yanajulikana na kwa kuwa polisi hao hao wanakamata watu inakuwa ngumu kujichunguza wao wenyewe na kujiamulia wakahukumiwe au la!,” amesema.
Amependekeza kiundwe chombo kitakacholidhibiti jeshi hilo, pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilichukulie suala hilo kwa uzito unaotakiwa kwa kufuatilia.
Jeshi la Polisi
Mkuu wa Sheria wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni amesema msingi wa kazi ya Jeshi hilo ni kufuata kanuni, sheria na taratibu za kijeshi zilizopo.
Amesema katika hilo rushwa ni adui, hivyo hawapaswi kupokea hata kidogo.
Amesema askari anafanya kazi kwa kufuata kanuni hizo na ieleweke aina yoyote iwe hisia, harufu au fikra ya rushwa ni marufuku kwa kuwa misingi ya kazi inakataza.
“Kwetu hatuna samahani na askari yeyote anayejihusisha na rushwa, adhabu yake ni kufukuzwa kazini kisha taratibu zingine za kisheria kufuatwa,” amesema Sokoni.
Amesema rushwa ni adui wa haki na wajibu wao wa msingi kama Jeshi la Polisi katika kulinda raia na mali zao ni kuhakikisha wanasimamia haki itendeke katika maeneo wanoyasimamia.
Sokoni amesema watumiaji wote wa barabara wajue kuwa rushwa ni adui wa haki na wanatakiwa watimize wajibu wao wa msingi, hivyo wasishawishi wala kuitoa kwa askari.
Katika kupambana na rushwa amesema Serikali imekuja na utatu ambao ni Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wadau wa usalama barabarani ili kupiga vita rushwa ya barabarani ambayo inaweza ikawa chanzo cha ajali.
Ametoa rai kwa askari yeyote anayejihusisha na rushwa wananchi watoe taarifa.
Amesema mpango wa utatu umeshatenda kazi, ikiwemo kuwafukuza kazi baadhi ya askari.