Wadau wanolewa kuzingatia sheria matumizi ya mtandao
Muktasari:
- Wadau wa habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii wametakiwa kuzingatia sheria za matumizi ya mitandao ili kuepusha kuingia matatani pale wanaposambaza taarifa zisizo na ukweli au kudhalilisha utu wa mtu.
Mwanza. Wadau wa habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii wametakiwa kuzingatia sheria za matumizi ya mitandao ili kuepusha kuingia matatani pale wanaposambaza taarifa zisizo na ukweli au kudhalilisha utu wa mtu.
Hayo yamebainishwa leo Jumamosi Mei 5, 2021 katika mjadala wa sheria ya matandao na uhuru wa kujieleza uliofanyika katika Chuo Kikuu Saut jijini Mwanza na kuhusisha wanafunzi wa kitivo cha sheria, habari na mawasiliano ya umma yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan).
Katika mdahalo huo Jaji Adam Mambi alitoa mafunzo sambamba na Michael Baruti na wakili Mwasi Mbegu.
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya umma wa chuo hicho, Dk Peter Mataba amesema madhara ya kusambaza taarifa ambazo hazina ukweli ni makubwa lazima watumiaji wa mitandao ya kijamii kuzingatia sheria.
Amesema licha ya kuwepo kwa sheria lakini baadhi ya watu wanatumia mitandao kuwadhalilisha wengine au taasisi.
“Lazima watu wabadilike na kutambua kuwa kutuma ujumbe usio na ukweli au kutothibitishwa ni makosa kisheria, tunapaswa kuwa na uadilifu tunapotumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia haki za watu, nishauri elimu iendelee kutolewa” amesema Mataba.
Keneth Kusanda ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho wameshauri wadau wa habari kuzingatia na kufuata maelekezo ya matumizi ya mitandao na kwamba sehemu yenye kubana haki ya kujieleza ifanyiwe marekebisho.
“Japo tunataka uhuru wa kujieleza lakini kuna kikomo chake, sio kila kitu kiwe kusambazwa bila kuzingatia sheria na kama kuna upungufu urekebishwe kwa maslahi ya pande zote ila kimsingi sheria izingatiwe” amesema Kusanda ambaye ni Mwanafunzi wa Sheria.
Ofisa mradi wa Misa-Tan, Lucy Kilanga amesema wataendelea kutoa elimu nchi nzima hasa kwa waandishi wa habari, wadau wa habari na wanasheria ili kujenga jamii yenye kutambua sheria za mitandaoni.
“Lengo letu ni kuwapa elimu wanafunzi hawa wa idara ya habari na mawasiliano ya umma, lakini pia wanasheria kuhakikisha wote kwa pamoja kama wahusika wanaelewa misingi na sheria za matumizi ya mitandao, tutaendelea kutoa elimu kwa nchini nzima” amesema Kilanga.