Wadau wataja sababu kuadimika mafuta ya kula nchini

Wadau wataja sababu kuadimika mafuta ya kula nchini

Muktasari:

  • Kutokuwa na uwekezaji mkubwa wa viwanda vya usindikaji na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana zimetajwakuchangia kupanda kwa bei ya mafuta ya kula nchini.
  • Wakati wadau wakieleza hayo meli iliyobeba shehena ya mafuta hayo itaanza kushusha tani 26,450 leo baada ya ile iliyokuwa ana tani 21,800 kumaliza kushusha Januari 4.

Dar/ Dodoma. Kutokuwa na uwekezaji mkubwa wa viwanda vya usindikaji na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana zimetajwa kuchangia kupanda kwa bei ya mafuta ya kula nchini Tanzania.

Wakati wadau wakieleza hayo meli iliyobeba shehena ya mafuta hayo itaanza kushusha tani 26,450 leo baada ya ile iliyokuwa ana tani 21,800 kumaliza kushusha Januari 4.

Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 na kiasi kinachozalishwa nchini ni tani 205,000 hivyo kuwa na upungufu wa tani 365,000 ambazo huagizwa kutoka nje.

Wamiliki wa viwanda vya kukamua mafuta, wakulima na wanunuzi walisema mvua zilizonyesha mwaka jana hazikuwa rafiki kwa zao la alizeti kwani mbegu nyingi ziliozea mashambani na kusababisha hasara kwa wakulima.

Meneja wa kiwanda cha Mount Meru kilichopo Singida, Nelson Mwakabuta alisema msimu wa mwaka huu hawakupata mbegu za kutosha hivyo bei kupanda kwani wanalazimika kununua kwa wachuuzi waliozihifadhi.

Kwa sasa alisema wananunua kilo moja hadi Sh1,050 kutoka kati ya Sh600 hadi Sh700 hivyo kuwalazimu kupandisha bei ya mafuta hayo ili kufidia gharama.

“Hata sisi kiwandani tunalima alizeti kwa wingi lakini msimu uliopita hatukuvuna kwa kiwango tarajiwa kwani mbegu nyingi ziliozea shambani na wakulima wengi ikawa hivyo, sasa hivi tunapata kwa uchache kutoka kwa wajanja waliokuwa wameweka akiba ndiyo wanatuuzia kwa bei za kurusha,” alisema.

Meneja wa kampuni ya kilimo ya Jatu, Mohammed Simbano alisema kuadimika kwa mafuta kunatokana na kutokuwepo kwa wawekezaji wakubwa.

“Uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula hautoshelezi mahitaji, miongoni mwa sababu ni wakulima wengi kutofanya kilimo biashara, lakini tungekuwa tuna kampuni kubwa hata 10 tu, ambazo zinazalisha kwa kuzingatia mahitaji ya nchi tungeweza hata kuuza nje,” alisema.

Alfred Gwivaha mkulima wa alizeti Kijiji cha Pwaga wilayani Mpwapwa alisema mwaka huu ulikuwa mzuri kwa wakulima kwani wameuza alizeti kwa bei wanayoitaka wao bila kusumbuliwa licha ya kuwa zao hilo halikukomaa kwa kiwango kinachotakiwa.

“Ni kweli tumeuza kwa maringo, hata kama hayajakomaa we peleka sokoni wanagombania sasa unaachaje kupandisha bei wakati misimu mingine walikuwa wanatusumbua kuchagua aina ya mbegu wanayotaka kununua,” alisema.

Hivi karibuni Waziri Mwambe alisema kuna meli mbili zimeingia Bandari ya Dar es Salaam kushusha mafuta ya kula.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta wa pamoja (PBPA), Erasto Mulokozi alisema meli ya kwanza ilimaliza kushusha mzigo tangu Januari4 na nyingine inatarajia kuanza kushusha jana.

“Meli moja ilianza kushusha mzigo Desemba 29 mwaka jana na imemaliza Januari 4, Nyingine ilipangiwa kuanza kushusha Januari 19, lakini tumefanya mabadiliko ya ratiba itaanza kushusha leo (jana) na itachukua siku tatu,” alisema Mulokozi.

Alisema sheria yetu inasema kipaumbele kitolewe kwa meli zinazoshusha mafuta ya kuendesha mitambo kama Petroli na dizeli lakini kam sehena ya bidhaa hizo ipo ya kutosha na hizo zinazoshusha aina nyingine ya mafut zinapewa kapaumbele.

“Licha kuwa kipaumbele ni mafuta ya mitambo lakini kama akiba iliyopo nchini inatoshereza mahitaji yasisyopungu siku 15 tuntoa nafasi kwa mafuta mengine na ndicho tulichokifanya sasa meli ya pili ilitakiwa ishushe tarehe 19 lakini tumeivuta mpaka leo,” alisema.

Aidha Mwambe alisema Wizara imewekeza nguvu katika Mkoa wa Kigoma kuhusu ushiriki wa Taasisi za Umma katika uzalishaji wa mchikichi kwa ajili ya usindikaji wa mafuta, Sanjari na kuendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vikubwa, vya kati na viwanda vidogo ili kutatua tatizo la uhaba wa mafuta ya kula nchini.

Imeandikwa na Ephrahim Bahemu na Habel Chidawali, [email protected]