Wadau wataja sababu zinazochangia ukatili kwa watoto
Msimamizi wa masuala ya jinsia kutoka Shirika la Plan international linalotekeleza Mradi wa kuwawezesha wasichana wa rika balehe kuendelea na masomo (Kagis), Hildegada Mashauri akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa masuala ya watoto wa mikoa ya Geita na Kigoma yaliyofanyika mkoani Kigoma.
Muktasari:
- Wakati taarifa za Jeshi la Polisi nchini zikionyesha matukio ya ukatili kwa watoto ni 12,163 kwa mwaka 2022, wadau wa masuala ya watoto kutoka mikoa ya Kigoma na Geita wamesema kutowajibika kwenye malezi na makuzi yao ni miongoni mwa sababu zinazochangia wengi wao kukosa ustawi mzuri na kuchangia vitendo vya ukatili.
Kigoma. Wazazi na walezi kutowajibika kwenye makuzi ya watoto kumetajwa kuwa miongoni mwa sababu za watoto kukosa misingi mizuri ya ustawi na kupelekea kushamiri kwa vitendo vya ukatili na endapo juhudi za maksudi hazitachukuliwa ipo hatari ya Taifa kushindwa kufikia maendeleo endelevu.
Wakizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wanaoshughulika na masuala ya watoto yaliyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la Plan International kupitia mradi wake wa kuwezesha watoto wa kike kuendelea na masomo (Kagis), wamesema bado elimu inahitajika kwenye jamii juu ya makuzi sahihi ya mtoto.
Msimamizi wa masuala ya jinsia kutoka Shirika la Plan Interinational linalotekeleza mradi wa kuwawezesha wasichana wa rika balehe kuendelea na masomo (Kagis), Hildegada Mashauri amesema kwenye jamii ipo changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya ukatili wa kijinsia na matokeo yake yanawaathiri watoto.
“Mradi wetu wa Kagis wa kumuendeleza mtoto wa kike kuendelea na masomo unamuwezesha msichana kupata uelewa wa masuala ya ukatili, atambue akifanyiwa ukatili aende wapi ajue ukatili ni nini na haki zake ni zipi lengo ni kuwa na jamii yenye uelewa inayotoa pia taarifa za ukatili wa kijinsia,” alisema.
Amesema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya watu wa Cananda katika mkoa wa Kigoma na Geita umewakutanisha wataalamu hao ukiwa na lengo la kuhakikisha jamii hasa ya wasichana wanapata ulinzi na usalama na kuishi kwenye mazingira huru ambayo hayana ukatili wa kijinsia.
Amesema kesi nyingi za ukatili hukosa ushahidi na sababu kubwa ni uelewa mdogo wa jamii juu ya masuala ya ukatili pamoja na kutojua hatua za kufuata pindi mtu anapofanyiwa ukatili.
“Kutokujua hatua za kufuata sio tuu kunamnyima mhanga wa ukatili haki kwenye vyombo vya sheria, bali pia inaweza kusababisha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kama hatapata huduma ndani ya saa 72,” amesema.
Akizungumzia sababu za kesi nyingi za ukatili ikiwemo zile za ubakaji kushindwa kumtia hatiani mshatakiwa Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Johari Kijuwile alisema chanzo ni ushahidi hafifu pamoja na kasoro mbalimbali wakati wa upelelezi wa kesi hizo.
“Mara nyingi upande wa upelelezi una acha watu muhimu kwenye ushahidi mfano mtoto amebakwa haletwi mahakamani kutoa ushahidi wanamaliza kifamilia kesi italetwa mahakamani itatajwa lakini mwisho wa siku itatupiliwa mbali na jamii itaona haki haitendeki,” alisema Kijuwile.
Taarifa za Jeshi la Polisi nchini za mwaka 2022 zinaonyesha matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa 12,163 na kati yao 9,962 ni watoto wa kike.
Takwimu hizo zinaonesha matukio ya ukatili dhidi ya watoto yaliyoongoza ni pamoja na ubakaji 6,335, ulawiti 1,555, mimba za utotoni 1,557, kuzorotesha masomo 808 na mashambulizi yalikua 231.