Wadau watia neno uboreshaji daftari la wapigakura

Muktasari:

  • Wadau wa vyama siasa wametoa maoni tofauti juu ya mchakato wa kuboresha daftari la kudumu la wapigakura unaofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ambapo majaribio yataanza Novemba 24 hadi 30, 2023 katika kata mbili za Ng'ambo iliyopo Tabora Mjini na Ikoma iliyopo Rorya mkoani Mara.

Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano wa kitaifa wa Tume ya Uchaguzi na Vyama vya Siasa kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari hilo.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika leo Novemba 16, 2023, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jacob Mwambegele amesema majaribio hayo yatahusisha vituo 16 vya uandikishaji ambapo 10 vitakuwa katika Kata ya Ng'ambo na vituo sita katika Kata ya Ikoma.

Amesema huko nyuma walitumia mashine za ‘biometric’ (BVR) katika kuandikisha wapigakura na kwamba mashine hizo zilikuwa na uzito wa kilo 35, jambo ambalo lilisababisha changamoto katika kuzihamisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Hata hivyo, sasa amesema watatumia mfumo wa ‘VRS’ ambao mashine zake zina uzito wa kilo 15 na zinatumika Android badala ya Window ambayo ilikuwa ikitumika huko nyuma.

"Shughuli hii itawahusu waliofikisha miaka 18 hadi kufikia tarehe ya uchaguzi, wanaotaka kubadilisha au kuhamisha taarifa zao na kuwaondoa waliopoteza sifa za kuwa wapigakura.

"Vyama vya siasa vitaweka mawakala kwenye kila kituo cha uchaguzi wakati wa majaribio," amesema Mwambegele huku akivitaka vyama hivyo vya siasa kuwahamasisha wanachama wao kujitokeza wakati wa Majaribio hayo na hivyo kujiandikisha kwenye daftari hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Ramadhan Kailima ameeleza sababu za kuchagua kata hizo kuwa ni ongezeko la idadi ya watu katika kata hizo, miundombinu ya mawasiliano na mwingiliano wa watu hususani kule Rorya ambako ni mpakani.

Ameeleza pia madhumuni ya majaribio hayo kuwa ni kupima uwezo na ufanisi wa vifaa vitakavyotumika na pia kubaini changamoto zitakazojitokeza na kutafuta utatuzi wake.

Wakizungumzia mchakato huo, wadau wa vyama siasa wametoa maoni tofauti huku wengine wakihoji kuchelewa kwa shughuli hiyo ambayo kwa mujibu wa sheria unatakiwa kufanyika mara mbili ndani ya miaka mitano.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema uboreshaji wa daftari la kudumu umechelewa kwa kwa kuwa ulipaswa kuwa umefanyika na sasa Tume ingejielekeza kujiandaa na awamu ya pili ya uboreshaji kabla ya kwenda kwenye uchaguzi.

Hata hivyo, Mnyika amesema mchakato huo unapaswa kusitishwa kwa sababu tayari Sheria ya Tume ya Uchaguzi ipo kwenye mchakato wa kufanyiwa mabadiliko, hivyo anadhani ni muhimu kazi hiyo ikafanywa na Tume mpya itakayopatikana katika sheria itakayopitishwa.

"Wadau tumekuwa hatuna imani na hii Tume, mchakato wa uchaguzi unaanza kwenye uandikishaji wa wapigakura. Nadhani ni busara shughuli hii ingesitishwa kwanza hadi Tume mpya itakapopatikana," amesema.

Naye Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ametaka shughuli ya uandikishaji wa wapigakura ikasitishwa hadi mchakato wa mabadiliko ya sheria za uchaguzi utakapokamilika.

"Ni vizuri shughuli hii ikasimamiwa na chombo kinachoaminiwa na kukubaliwa na wadau wote ambacho kitapatikana baada ya kukamilika kwa mabadiliko ya sheria zote zinazosimamia uchaguzi," amesema Shaibu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo ametaka wafungwa na Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) nao waruhusiwe kujiandikisha na kupiga kura kwa sababu nao ni Watanzania na wana haki kama wengine.

"Hakuna haja ya kuwabagua wafungwa na diaspora, kwenye huu uboreshaji nao waruhusiwe kwa kuwa ni Watanzania. Tukifanya hivyo tutakuwa tumepanua wigo wa demokrasia nchini.