Wadau watoa angalizo kutoweka kwa punda nchini

Wadau watoa angalizo kutoweka kwa punda nchini

Muktasari:

  • Wadau wa sekta ya mifugo nchini Tanzania wamesema kama Serikali isipoingilia kati kuratibu biashara ya nyama ya punda miaka michache ijayo wanyama hao watatoweka nchini.

Arusha. Wadau wa sekta ya mifugo nchini Tanzania wamesema kama Serikali isipoingilia kati kuratibu biashara ya nyama ya punda miaka michache ijayo wanyama hao watatoweka nchini.

Wakizungumza leo Jumapili Desemba 13, 2020 katika kikao cha wadau wa sekta ya mifugo jijini Arusha, wameeleza kuwa punda wamekuwa wakinunuliwa vijijini kwa wingi na hivyo kupunguza nguvu kazi ya kilimo, kutafuta maji na kusafirisha mizigo.

Mkurugenzi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii Afrika (Inades),  Herman Hishamu amesema kuwa idadi ya punda nchini ni takriban 660,000 na kwamba

mnyama huyo hutumika zaidi na watu wenye kipato cha chini kwa ajili ya kulima pamoja kubeba mizigo.

Amebainisha kuwa hivi karibuni imeibuka biashara ya nyama ya punda inayofanywa na kampuni mbalimbali na kupeleka nje ya nchi sambamba na kununua wanyama hao hasa mkoani Shinyanga.

“Mwaka huu wamenunua punda 88,000, kule Iringa wanapeleka watu hospitali kutumia usafiri wa punda  hivyo tungeomba biashara hiyo isitishwe kwani imekuwa kilio kikubwa,” amesema.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ameahidi kuanza kufuatilia kupotea kwa wanyama hao kutokana ongezeko la viwanda vya kuchinja.

“Nimepokea hilo naahidi changamoto zote tutazifanyia kazi kuhakikisha sekta hii ya mifugo inakuwa sekta ya mfano wa kuigwa kwani wananchi wengi wamekuwa wakitegemea sana wanyama kazi hawa,” amesema.

Amesema wizara ipo kwenye mchakato wa kuanzisha chanjo kwa mifugo itakayoanza  kutolewa Februari 2021 na itasimamiwa na wizara hiyo na si halmashauri.

Ofisa mkuu Wizara ya Kilimo,  Lameck Hazari amesema  kilimo kinahitaji uwepo kwa wanyama kazi kwani hutumika kwa asilimia 27 wakati trekta ni asilimia 20 tu.

___________________________________________________________________

Na Husna Issa ,Mwananchi [email protected]