Wafanyabiashara 45 wa Tanzanite wahamia Mirerani

Muktasari:

  • Wanunuzi wakubwa 45 wa madini ya Tanzanite wamefungua ofisi za kununua madini katika Mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Mirerani. Wanunuzi wakubwa 45 wa madini ya Tanzanite wamefungua ofisi za kununua madini katika Mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea Mirerani Julai 7, 2021 na kuagiza biashara ya madini ya Tanzanite ifanyike Mirerani pekee kuanzia Julai 10 mwaka huu uamuzi ambao umetekelezwa.

Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, Caroline Mthapula akizungumza na makatibu wakuu nane walipotembelea eneo hilo leo Jumatano Novemba 10 amesema wafanyabiashara 45 wameshafungua ofisi zao Mirerani.

Naye, Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amesema mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo katika mji mdogo huo na nchi kwa ujumla.

"Mradi utaongeza kipato kwa wananchi, ajira, kutambulika kwa Mirerani kidunia na kuongezeka kwa miundombinu na," amesema Makongoro.

Naye, Katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema makatibu wakuu hao wamefika Mirerani ili kushuhudia utendaji kazi unaoendelea.

Profesa Msanjila ametaja baadhi ya makatibu wakuu hao ni Wizara za Tamisemi, Madini, Maji, Ardhi, Nishati, Biashara, Sheria na Katiba.