Wafanyabiashara waandamana Mbeya

Baadhi ya wafanyabiashara wakiwa nje ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya baada ya vibanda vyao kubomolewa usiku wa kuamkia leo

Muktasari:

Pamoja na kuamdamana lakini hawakufanikiwa kumkuta Mkuu wa Mkoa huo baada ya kuambiwa kiongozi huyo yupo nje ya ofisi kwa kazi za kiserikali wilayani Chunya.

Mbeya. Zaidi ya wafanyabiashara 40 katika Soko Kuu mtaa wa Sokoine jijini Mbeya wameandamana katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kutoa kilio chao baada ya vibanda vyao kubomolewa usiku wa kuamkia leo Alhamisi Septemba 22, 2022 na watu wasiojulikana.

 Pia, imeelezwa katika bomoabomoa hiyo, mali za wafanyabiashara hao ambazo bado hazijajulikana thamani yake zimepotea na kuwaacha wafanyabiashara kwenye sintofahamu.

Habari zimeeleza kabla ya kubomoa vibanda hivyo wafanyabiashara walipewa notisi ya siku 90 na Halmashauri ya Jiji kuhama eneo hilo, ambapo wao walienda mahakamani kuweka zuio ambapo hukumu ilipaswa kutoka Oktoba 4 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Wakizungumza katika eneo la tukio, baadhi ya wafanyabiashara wamesema wameshtuka na uhalifu waliofanyiwa kwa kuvamiwa maeneo ya biashara na kuharibiwa mali zao.

"Huu ni uvamizi, kesi bado ipo mahakamani, tunaamka asubuhi tunakuta vibanda vyetu vimebomolewa, bidhaa zetu zimepotea sasa sijui wanataka tuishije" amesema Hussein Hamis.

Neema Mapunda amesema kilichofanyika ni nguvu na kwamba hawajui hatma yao kwani wana majukumu ya kifamilia na mikopo huku akihoji fidia kwa wahanga.

"Nichukue bakuli niende kuwa ombaomba? Hii hasara wataifidia? Watatupeleka wapi? Tuna mikopo, tunasomesha watoto yaani wametumia nguvu" amesema Neema.

Baadhi ya vibanda vinavodaiwa kubomolewa na kusababisha wafanyabiashara kuandamana mpaka kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya

Diwani wa Sisimba, Josephine Kamuga amesema alipata taarifa kuhusu sakata hilo ambapo aliliwasilisha kwenye kikao cha madiwani na kumuuliza Mkurugenzi wa Jiji kuhusu suala hilo na hatma ya wafanyabiashara hao na kujibiwa kuwa walishapewa notisi ya siku 90 kuhama hapo na watapelekwa Old Airport hadi ujenzi wa vibanda vya muwekezaji vitakapokamilika watarudi.

"Lakini nikamuuliza kwamba hawa mkiwafukuza wataenda wapi ilhali wengine wana mikopo? Leo ndio naamka nakutana na taarifa hizi za kubomolewa vinanda nikamuuliza mbona uvunjaji umekuwa wa usiku? Niwaombe tuwe watulivu andikeni majina yenu ndani ya siku mbili tujue tunalimalizaje" amesema Diwani huyo.

Hata hvyo, baada ya wafanyabiashara hao kufika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hawakufanikiwa kuonana naye baada ya kuambiwa kiongozi huyo yupo nje ya ofisi kwa kazi za kiserikali wilayani Chunya.

Mwananchi Digital ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Benjamin Kuzunga simu yake ilipokelewa na msaidizi wake akisema kamanda yupo kwenye kikao.