Wafanyakazi wa Azania Benki wawakumbuka watoto yatima, wanaoishi katika mazingira magumu
Moshi. Katika kusheherekea sikukuu ya Eid el Fitr, Wafanyakazi wa Benki ya Azania, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wametoa msaada wa vyakula ikiwemo mbuzi, mchele na mafuta kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu na yatima katika shule ya wasichana ya Uchira Islamic iliyopo wilayani humo.
Akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo leo, Meneja wa benki ya Azania wilayani humo, Yusuf Kilenga amesema kama jamii wanaowajibu wa kuwakumbuka watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuifanya na wao kuwa sehemu ya watu wenye furaha hasa katika sikukuu hii ya Eid el fitr.
"Sisi kama wafanyakazi wa benki ya Azania hapa Moshi leo tumeona tutoe kidogo tulichonacho kwa jamii, hasa katika shule hiii ambayo tumeambiwa ina watoto wenye uhitaji maalumu,"
"Kama sehemu ya kusherekea sikukuu ya Eid El fitr tumeona tuje kwa hawa watoto wetu ili na wao wajione hawajaachwa na waione siku hii ni muhimu kwao, hivyo tumeona tusambaze furaha kwa hawa watoto wetu na wadogo zetu, hivyo leo tumewaletea mchele , mafuta na mbuzi ili kuifanya siku hii kuwa nzuri kwao,"
Akipokea misaada hiyo ya vyakula , Mkuu wa shule hiyo, Abdulkahar Mfinanga, amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 412 miongoni mwao wakiwemo watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, ambao amesema msaada huo wa vyakula utawafanya wanafunzi hao kusheherekea vizuri sikukuu ya Eid.
"Shule hii ina wanafunzi 412 na ni shule ambayo imekaa kijamii zaidi hasa kwa wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu na watoto yatima, kwa kweli zawadi hii tuliyoletewa leo ni fahari kubwa kwetu na Benki hii wametupa faraja kubwa,"amesema Mwalimu Mfinanga
Akiishukuru benki hiyo, amewaomba wadau wengine wenye moyo wa kutoa kwa ajili ya kuisaidia jamii kujitokeza kusaidia shule hiyo kwa kuwa ina uhitaji mkubwa wa misaada mbalimbali kwa kuwa inawalea wanafunzi wenye uhitaji maalum na yatima.
"Tunaishukuru Benki ya Azania kwa kutukumbuka , wametuonyesha upendo mkubwa na wakawafanya watoto wetu hawa kuona kwamba jamii haijawasahau na kuifanya siku yao ya Eid kuwa siku ya furaha,"
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Bilhis Mohammed, ameishukuru benki hiyo na kusema wamewatia moyo kwamba wapo watu ambao wanawakumbuka watu ambao wanauhitaji maalum kwa jamii.
"Tunashukuru kwa hiki ambacho tumeletewa maana na sisi tumeona kwamba ipo jamii ambayo inatukumbuka, hili ni jambo la kheri kwetu na leo siku yetu tunaisherekea vizuri, kwa hiyo wametupa moyo kwamba jamii inatukumbuka,"