Wafanyakazi wa ndani wataka kuheshimiwa

Wednesday May 25 2022
wafanyakazi pic
By Shakila Nyerere

Dodoma. Wafanyakazi wa majumbani wameomba mkataba namba 189 uridhiwe na Serikali huku wakiwaomba waajiri wao kuwaheshimu kwani wao ni zaidi ya walezi katika familia.

Kilio hicho wamekitoa leo Jumatano Mei 25, 2022 katika mkutano wa wafanyakazi wa majumbani ulioandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa Mahotelini, Mashambani na Majumbani (Chodawu).

Mariamu Mwaramu amesema changamoto kubwa ambazo wamekuwa wakikutana nazo ni pamoja na kutokuheshimiwa, kutokupewa muda wa mapumziko, udhalilishwaji wa kingono, kutokupewa likizo ya uzazi, kutoaminiwa kutokupewa mshahara kwa wakati na kukashifiwa.

“Hatuna Jumapili wala Jumamosi muda wote sisi ni kufanya kazi, ukisema nikaangalie ndugu ni shida, mshahara wenyewe hupati kwa wakati ukisema uombe ndio shida inaanzia hapo hapo,”amesema.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuridhia mkataba namba 189 kwani una vitu vingi ambavyo vitawafanya wao wapate baadhi ya haki zao.

Betrice John ambaye anafanya kazi za ndani mkoani Morogoro amesema wamekuwa hawathaminiki katika jamii hadi kufikia kupewa majina ya udhalilishaji kama beki tatu.

Advertisement

“Tumesahaulika tunaomba tusikilizwe hata kidogo mkataba urithiwe ili tutambulike. Sisi ni walimu sisi ni madaktari japokuwa hatuna vyeti watoto wakianza kuumwa sisi ndio huwa tunaanza kuwahudumia tunaomba tuheshimike,”amesema.

Katibu Mkuu wa Chodawu Tanzania Bara, Said Wamba amesema wanaiomba Serikali iweke sheria madhubuti kwa wafanyakazi wa majumbani kwani wamekuwa watu muhimu katika jamii.

Wamba ametoa rai kwa wafanyakazi wa majumbani kujiunga na chama ili iwe rahisi kutetea maslahi yao pamoja na kupaza sauti kwa chochote kitakachotokea kwao.

Advertisement