Wafugaji waiangukia Serikali ubora vifaranga, vyakula vya kuku

Muktasari:

  • Kutokana na vifo vya vifaranga vinavyotokea kwenye mabanda na vyakula kushindwa kukuza kuku kwa muda unaotakiwa, wafugaji nchini wameiomba Serikali kudhibiti kampuni zinayotoa vifaranga na vyakula vya kuku wa nyama visivyo na ubora kwani vinawadidimiza kiuchumi.

Arusha. Kutokana na vifo vya vifaranga vinavyotokea kwenye mabanda na vyakula kushindwa kukuza kuku kwa muda unaotakiwa, wafugaji nchini wameiomba Serikali kudhibiti kampuni zinayotoa vifaranga na vyakula vya kuku wa nyama visivyo na ubora kwani vinawadidimiza kiuchumi.

Hayo yamesemwa na wafugaji hao leo Jumapili Novemba 20, 2022 kwenye mkutano wa siku moja uliowakutanisha wafanyabiashara wa kuku na wafugaji kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga na Dodoma.

 Mmoja wa wafugaji hao, Beatrice Mlay kutoka Moshi anayefuga kuku 500 amesema ufugaji wa kuku umekuwa na changamoto nyingi zinazokatisha tamaa ya kuendesha shughuli hiyo huku baadhi ya kampuni wakitoa bidhaa zisizo na ubora hali inayowadidimiza kiuchumi.

"Miaka ya nyuma ufugaji ulikuwa unalipa sana kiasi cha kuwa shughuli ya kipaumbele kwa vijana wasio na ajira au wazee wanaostaafu lakini kwa sasa imekuwa inatunyonya hata mitaji yetu kutokana na baadhi ya kampuni kutokuwa waaminifu na bidhaa wanazotuuzia kwa kupunja baadhi ya virutubisho kwenye vyakula ili kujipatia faida" alisema na kuongeza


"Tunaomba Serikali ifanye msako wa viwanda vya vyakula bubu na wale wanazotengeneza vyakula vizivyo na ubora pia mashamba makubwa ya kuzalisha vifaranga wakaguliwe maana siku hizi vifaranga vingi feki havina ubora, vinakufa vikifika bandani na wengine kudumaa bila kukua kwa muda tarajiwa," amesema


Amesema katika banda lake analoingiza kuku 500 kuanzia siku ya kwanza hadi siku 35 anayopaswa kuuza, hupoteza zaidi ya kuku 50 hadi 100 inayotoka na vifaranga dhaifu na vyakula visivyo bora.


Kwa upande wake, Charles Shauri anaefuga kuku 1000 amesema  changamoto inayowakabili ni bei ndogo ya kuku ya Sh7,000 kwa mmoja huku kukiwa na bei kubwa ya vyakula vya kuku wa nyama.


"Tatizo ni uhaba wa nafaka na protini iliyotokana na kukumbwa na mabadiliko ya tabia ya nchi hasa ukame kiasi cha wafanyabiashara wa chakula kutupandishia bei kulingana na wanavyopata lakini kupunja baadhi ya protini na virutubisho kwenye kuchanganya vyakula hii inawafanya kuku kuishi bandani kwa zaidi ya siku tano hadi 10 za ziada kutoka ile 30 hadi 35 anayopaswa kuuzwa," amesema


Meneja wa kampuni ya bidhaa za kuku kutoka trouw Nutrition, Joseph Joachim amesema wako jijini Arusha kuwapa mafunzo zaidi wafugaji jinsi ya kutumia bidhaa za asili kutoka vya mimea na matunda kukuzia kuku bila dawa zenye kemikali zinazoathiri zaidi walaji wao ambao ni binadamu.


Amesema changamoto kubwa katika ufugaji ni magonjwa mbalimbali yanayowapata kuku inayotoka na asili ya kifaranga alipototolewa, hali ya hewa, maji na chakula hasa visivyo na virutubisho vya kutosha au vilivyopatwa na ugonjwa sumu kuvu.


"Haya yote yanawalazimu wafugaji kutumia dawa nyingi hata yaliyo hatari kwa walaji kwa kusababisha magojwa ya kansa lakini watatumia kuokoa kuku wao.

“Kutokana na hilo tumekuja kuwapa Suluhu la bidhaa kadhaa za kuwasaidia kutibu kifaranga akiwa mdogo, maji yao ya kunywa lakini pia virutubisho mbalimbali vya chakula ili kuokoa kuku kudumaa na hizi hazina madhara wala kemikali," amesema


Amesema sekta ya ufugaji wa kuku inakua zaidi nchini kutoka kuku milioni 44 kwa miaka mitano iliyopita hadi milioni 92.


Kwa upande wake, mtaalamu wa mifugo kutoka chuo cha mifugo lita, Benovita Balama amesema ubora wa chakula vya kuku vinatokana na vingi kutengenezwa mtaani bila kuzingatia kanuni za uzalishaji bora huku baadhi ya wafanyabiashara wakitumia bidhaa zilizovunda hasa mahindi na maharage.


"Kwa sasa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kuna uhaba mkubwa wa chakula nchini hivyo wafanya biashara wengi hununua nje lakini kwa kushindwa kuhifadhi vema vinavunda na kuitengeneza sumu kuvu ambayo ni hatari Sana kwa mifugo," amesema