Wafungwa gereza la Karanga wapatiwa sadaka ya futari
Moshi. Wakati waumini wa dini ya Kiislam nchini wakitimiza siku 22 za mfungo wa Ramadhan, Mbunge Mstaafu wa Moshi mjini, Jaffary Michael amewaasa wananchi kuwa na tabia ya kuwatembelea wafungwa waliopo magereza kama moja ya sadaka kwa Mwenyezi Mungu.
Hayo aliyasema jana, wakati akikabidhi shehena ya vyakula mbalimbali, ikiwemo mchele, unga wa ugali, tambi pamoja na mafuta ya kupikia kwa Mkuu wa gereza la Karanga lililopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza kwa niaba ya mbunge huyo mstaafu, Katibu wake, Deogratius Kiwelu alisema kuwakumbuka wafungwa waliopo magereza ni moja ya thawabu kubwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa wao ni binadamu kama walivyo binadamu wengine na kwamba wapo magereza kwa ajili ya kujifunza.
"Leo mheshimiwa mbunge ameleta vyakula kwa ajili ya kuwasaidia wafungwa waliopo katika gereza hili la Karanga, kwasababu anaamini kwamba binadamu yeyote anaweza kufungwa kwa wakati wowote,"
"Hawa waliopo gerezani ni ndugu zetu na kila mwaka lazima alete vyakula hapa kwa ajili ya futari na pasaka , tumeleta unga, mchele, tambi, mafuta ya kupikia, kwa ajili ya kuwasaidia wenzetu hawa ambao baadhi yao wako kwenye mfungo,"
"Tunajua wapo watu wenye uwezo na hawa waliopo humu ndani ni ndugu zetu kwa hiyo wajitahidi mara kwa mara kuwaletea vyakula pamoja na mahitaji mengine kama nguo, magodoro, mashuka, vitabu vya dini vya kusoma , tuwasaidie kwasababu kila mtu yuko hapa kwa ajili ya kujifunza,"
Akipokea misaada hiyo kwa niaba ya Mkuu wa gereza la Karanga, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Frank Lukindo alimshukuru mbunge huyo mstaafu kwa misaada hiyo na kuiomba jamii kuendelea kuwaangalia wafungwa na mahabusu ambao wapo gerezani hasa katika mfungo huu wa ramadhani.
"Tunamshukuru Mbunge Mstaafu kwa msaada huu mkubwa ambao tumeletewa leo, lakini pia tunaiomba jamii iendelee kuangalia hawa watu jamii ya wafungwa na mahabusu ambao wapo katika gereza hili la Karanga,"
"Kuna ndugu zetu ambao wako kwenye mfungo wa ramadhani na huu msaada utaendelea kuwasaidia sana na kuwafanya kutimiza moja ya nguzo ya dini yao ya Kiislamu, tunawashukuru sana," alisema Lukindo