Wahamiaji haramu 63 wanaswa Mbeya

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urich Matei

Muktasari:

Jeshi la Polis Mkoa wa Mbeya limekamata watu 63 kutoka nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila vibali.

Mbeya. Jeshi la Polis Mkoa wa Mbeya limekamata watu 63 kutoka nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila vibali.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Jumatano Mei 25, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urich Matei amesema wahamiaji hao wamekamatwa ndani ya siku tatu kuaniza Mei 22, 2022 baada ya Jeshi  hilo kufanya  misako na doria katika maeneo ya mpakani Wilaya ya Mbarali, Mkola Wilaya ya Chunya na Mlima Nyoka Wilaya ya Mbeya.

Matei amesema wahamiaji haramu 63 wote waliokamatwa ni wanaume raia wa nchini Ethiopia ambapo katika mahojiano wameeleza kuwa walikuwa wakisafirishwa kuelekea nchini Malawi.

Pia, Kamanda Matei amesema kuwa Watanzania wawili wamekamatwa kwa kosa la kuwasafirisha wahamiaji hao.

Amesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwani ni kinyume cha sharia.

Amesema wanaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ili kuzuia na kudhibiti uingizaji na upitishaji wa bidhaa za magendo na usafirishaji haramu wa binadamu huku akiwataka wananchi kujikita katika biashara halali.