Wahamiaji haramu kuwaweka polisi kitanzini

Monday January 18 2021
Wahamiaji haramu pic

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (aliyevaa suti), akiangalia ramani ya kambi mpya ya Uhamiaji ya Boma Kichakamiba, iliyopo wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, ambayo inaendelea kujengwa. Waziri huyo alifika kambini hapo kwa ajili ya kufungua mafunzo ya uongozi kwa maofisa na askari wa uhamiaji katika kambi hiyo. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala.

Mkinga. Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, George Simbachawene ametaja aina mbili za vichochoro vinavyotumiwa kuwapitisha wahamiaji haramu baada ya mipaka kudhibitiwa na kuonya atachukua hatua dhidi ya maofisa wa Polisi na Uhamiaji wa maeneo ya mpakani yatakayobainika kutumika kutorosha watu hao.

Simbachawene ameahidi kuwachukulia hatua maofisa uhamiaji pamoja na askari polisi watakaobainika kuzembea pale wahamiaji haramu watakapokamatwa na kubainisha wamepitia kwenye maeneo yao.

Alitaja vichochoro vinavyotumika kuwaingiza nchini Tanzania watu ambao baadaye huelekea Afrika Kusini kuwa ni pamoja na Bahari ya Hindi ambako hutumia vyombo vya majini. Simbachawene alieleza kuwa mbinu nyingine ambayo hutumika kuwavusha ni ile ya mipakani kwa usafiri wa bodaboda. Alitaja vichochoro hivyo wakati akifungua mafunzo ya maofisa na askari wa idara ya uhamiaji katika kambi mpya ya iliyopo Kichakamiba Boma Wilaya ya Mkinga mkoani hapa juzi.

Alisema kila makundi ya wahamiaji yanapofanikiwa kuingia Tanzania ni lazima kunakuwa na mawakala wenyeji wanaoratibu usafiri, malazi na vyakula na kuwatahadharisha kuwa wote watajikuta mikononi mwa dola.

“Siamini kama wahamiaji hawa haramu wanaingia wanahifadhiwa na wanasafirishwa hadi wanakamatiwa Morogoro bila baadhi ya askari wa uhamiaji na polisi Tanga kujua...kuanzia sasa wakikamatwa Morogoro na tukabaini walipita Tanga, mtambue kwamba nitawafagia bila huruma,” alisema.

Akitoa taarifa za mafunzo hayo, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk Anna Makakala alisema yanajumuisha maofisa na askari 387 ambapo wanajifunza masuala ya uongozi na utawala pamoja na ulinzi na kujihami.

Advertisement

Kambi hiyo mpya ya idara ya uhamiaji ya Kichakamiba ambayo imetengewa eneo la ukubwa wa ekari 365 ilianza kujengwa Julai, 2020 na hadi sasa jumla ya Sh140.milioni zimetumika.

Advertisement