Wahitimu wa vyuo vikuu sasa waukimbilia ufundi simu Veta

Muktasari:

  • Wasomi 300 wajitosa kusomea ufundi huo chuo cha ufundi Veta.

Awali vijana watundu ndio waliojipambanua kama mafundi simu katika maeneo mbalimbali nchini.

Ungeweza kuzungumza na baadhi yao, ukawauliza walikopatia ujuzi huo, jibu la wengi lingeweza kukuacha hoi. Ukweli ni kuwa wao ni mafundi wasiokuwa na mafunzo rasmi.

Hata hivyo, hali sasa imebadilika; kushamiri kwa matumizi ya simu hasa za kisasa na simu hizo kuwa sehemu ya maisha ya wati wengi, ufundi simu unaonekana kuwa kimbilio la vijana wengi wakiwamo wahitimu wa elimu ya juu.

Katika mazingira ya uhaba mkubwa wa ajira, kwa nini wasomi wasichangamkie fursa za kupata ujuzi unaoweza kuwahakikishia sio kuajiriwa, lakini hata kujiajiri.

Takwimu zinaonyesha vyuo vya elimu ya juu nchini vinazalisha zaidi ya wahitimu 60,000 kwa mwaka wanaolazimika kuingia kwenye soko la ajira kunyang’anyana nafasi chache zinazopatikana. Katika hao wachache wanatajwa kujiongeza kwa kujiajiri.

Asante kwa Chuo cha Ufundi Veta Kipawa, ambacho kinachotoa mafunzo hayo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoendeshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ukiratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na kufadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Chuo hicho kilichojikita zaidi katika kutoa mafunzo ya Tehama kinatoa mafunzo ya ufundi simu ambayo yamewavutia vijana wengi wakiwamo waliomaliza vyuo vikuu ndani na nje ya nchi.


Simulizi ya Kwambiana na Amina

Kwa wewe mhitimu wa elimu ya juu. Umesoma na bado unalia kukosa ajira? Umejaribu ufundi au unafikiri safari imeisha kwa kupata shahada?

Soma simulizi hii ya James Kwambiana, msomi mwenye shahada ya uzamili katika fani ya sayansi ya kompyuta.

Anasema baada ya kuhitimu masomo yake miaka kadhaa iliyopita, alijaribu kutafuta maisha mtaani katika fani ya teknolojia ya habari, lakini bahati haikuwa yake.

Hakutaka kulalamika akiwa bado anasoma shahada yake ya kwanza,aliamia kujiongeza kwa kusoma masuala ya umeme na baadaye kufanikiwa kupata kazi kama fundi simu asiye na ujuzi wowote rasmi.

Kwambiana anasema alifanya kazi ufundi simu katika mojawapo ya kampuni kubwa ya simu za mkononi kwa miaka sita na mwaka 2018 alirejea na kuendelea na shughuli hiyo katika maeneo ya Buguruni.

Anasema aliposikia kuna ufadhili wa Serikali chuo cha Veta Kipawa, hakusita kuomba na kufanikiwa.

“Niliposikia kuna ufadhili wa mradi wa SDF, niliomba na kupata kusoma, nilipomaliza nikapata ajira katika mojawapo ya kampuni za simu. Sasa hivi ni mhandisi wa huduma za simu katika kampuni hiyo.

“Unaweza ukawa fundi lakini usijue kwa usahihi baadhi ya shughuli unazotakiwa kuzifanya, lakini sasa najua kitu gani natakiwa kukifanya na kwa muda gani.

‘‘ Niliamua kuomba kusomea programu hii ili niwe na utalaamu na mbobezi zaidi wa masuala ya simu,”anasema Kwambiana huku akiwataka vijana kuikimbilia kozi hiyo fupi kwa kuwa ina nafasi kubwa ya kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu.

Ukimuondoa Kwambiana aliyesoma katika Chuo Kikuu cha Cape Town na baadaye Chuo Kikuu cha Stellenbosch, vyote vya nchini Afrika Kusini, msomi mwingine aliyeona fursa kwenye ufundi simu ni Amina Rashid, mhitimu wa shahada ya uhandisi katika mawasiliano na vifaa vya kielektroniki kutoka Chuo Kikuu cha St Joseph.

“Kupitia mafunzo ya ujuzi nikishirikiana na wenzangu, nimeweza kufungua duka langu la kutengeneza simu eneo la Kariakoo, licha kuwa na shahada ya uhandisi, lakini niliamua kusoma tena ufundi. Nawashukuru Benki ya Dunia na TEA maana hatukulipa chochote wakati tukisoma,” anasema.


Ufundi wa viwango

Habib Mfaume ni fundi simu wa mtaani ambaye awali anasema alikuwa akiifanya kazi hiyo kwa hisia na sio ka utaalamu maalumu. Aliweza kutengeneza simu sio kwa sababu aliamini ana ujuzi, lakini alifanya pasipo kuwa na uhakika kwa asilimia 100.

“Mfano muda mwingine simu inazima mie naipiga moto ndicho ninachojua kabla ya kupata mafunzo haya. Mafunzo haya yamesaidia kujua tatizo halisi la simu iliyoharibika.

‘‘Sasa hivi watu wana imani nami, nimeweza kufanya kazi na kampuni mbalimbali za simu zinazoagiza simu nje na kuzileta hapa nchini,” anasema Mfaume.


Mkuu wa chuo afunguka

Mkuu wa Chuo cha Veta-Kipawa, Sospeter Mkasanga anasema mafunzo hayo ni mapya chuoni hapo na kupitia mradi wa TEA, wamefanikiwa kuwafundisha wanafunzi zaidi ya 400 kupitia programu ya kuendeleza ujuzi inayoifadhiliwa na Benki ya Dunia.

Anasema mafunzo hayo yanaleta taswira mpya katika sekta ya ufundi simu. Anasema awali mafundi simu walikuwa wanatekeleza majukumu yao bila kuwa ujuzi sahihi unaostahiki.

“Ufundi simu sasa hivi umebadilika na umekuwa na taswira tofauti.Tunawafundisha mafundi simu kupitia mtaala uliopitishwa na kupata ithibati ya Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi (Nacte).

“Mbali na ufundi simu pia wanafundishwa kuhusu utambuzi wa hatari na usalama kuhusu makosa ya mtandao. Tunaishukuru TEA kwa kutuwezesha kununua vifaa vya kisasa vya utengenezaji wa simu ambayo ni vigumu kwa mtu mmoja kumudu kuvinunua,” anasema Mkasanga.

Alisema wahitimu wao wakimaliza mafunzo hayo, moja kwa moja wanakwenda kujiajiri au kuajiriwa katika taasisi mbalimbali.Anasema asilimia kubwa wanajiajiri wenyewe kwa sababu miongoni mwao walikuwa mafundi lakini hawakuwa na ujuzi au utalaamu mahiri wa kutengeneza simu.


Maombi yamiminika

Mratibu wa miradi na shughuli za uzalishaji wa Veta, Charles Mapuli anasema baada ya kuutangaza kozi kwa njia ya mtandao, ndani wiki moja walipokea maombi ya zaidi ya watu 3000 waliokuwa wakihitaji kujifunza kozi hiyo. Lakini nafasi za mafunzo hayo walitakiwa watu 400 kupitia mradi wa SDF.

Anasema miongoni mwa vigezo ni umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24, uzoefu na asilimia 70 waliochaguliwa walikuwa tayari wana ujuzi kuhusu ufundi simu. Huku 3O ni wapya wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu pamoja na wenye mahitaji maalumu.

Kwa mujibu wa Mapuli, baada ya kumalizika kwa wale wanafunzi waliofadhiliwa na SDF kwa sasa, Veta inaendeleza na kozi hiyo na kwamba hadi sasa wanafunzi zaidi ya wanafunzi 150 wamesoma kozi hiyo kwa kujilipia wenyewe.

“Kila mwezi kuna darasa jipya la ufundi simu linaanza katika ngazi ya awali na wanafunzi kati ya 15 hadi 20 wanajitokeza kusoma.Tunapokea maombi kutoka mikoa mbalimbali pamoja na Zanzibar kwa sababu ni chuo pekee kinachofundisha,”

“Baadhi yao ni waajiriwa, waliomaliza kidato cha nne, mafundi wanaokuja kujiendeleza na wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu.Tunawafundisha katika maeneo tofauti ikiwemo kozi ya vifaa vya umeme vyote, ngazi ya pili ni namna ya kutambua na kutibu matatizo ya simu wanayosoma kwa wiki sita,’’ anasema.


Mfuko wa kuendeleza ujuzi

Mfuko huo unalenga mafunzo ya ujuzi katika sekta za kipaumbele za kilimo, utalii na huduma za ukarimu, uchukuzi, ujenzi na teknolojia. Veta ni miongoni mwa vyuo vilivyojengewa uwezo na Benki ya Dunia ikiwemo kupewa Sh128.8milioni kwa ajili kutekekeleza mpango huo kwa vijana 476.

Mkurugenzi mkuu wa TEA, Bahati Geuzye anasema mradi wa SDF unalenga kufadhili programu za ujuzi kwa wanufaika 30,000 hadi kufikia Juni mwaka 2022. Anasema katika awamu ya pili ya SDF jumla ya taasisi 81 zimenufaika kwa ufadhili wa Sh9.7bilioni za kuendesha programu za mafunzo ya ujuzi.