Waibua hoja ya ubaguzi kufutwa ada ya mitihani

Muktasari:

Uamuzi wa Serikali kutangaza kufuta ada za mitihani kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne na sita kwa shule za umma, umepokelewa kwa mitizamo tofauti, huku baadhi ya wadau wakisema hatua hiyo inalenga kuonyesha tawala za kibaguzi.



Dar/Zanzibar. Uamuzi wa Serikali kutangaza kufuta ada za mitihani kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne na sita kwa shule za umma, umepokelewa kwa mitizamo tofauti, huku baadhi ya wadau wakisema hatua hiyo inalenga kuonyesha tawala za kibaguzi.

Tangu Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) lilipotangaza uamuzi huo Septemba 15, mwaka huu, wadau wamekuwa wakijadili suala hilo kwamba kwa nini linawabagua wanafunzi wanaosoma shule binafsi, wakati wote ni Watanzania.

Katika mitandao ya kijamii, mjadala umekuwa ukishika kasi, baadhi waliozungumzia suala hili ni viongozi wa dini walihoji, “kodi tulipe sote, ila wanaufaika ni baadhi ya Watanzania.”

Tangazo hilo la Necta kufuta ada hizo lilisema, “Baraza la Mitihani la Tanzania linawajulisha watu wote kuwa ada ya mtihani kwa watahiniwa wa darasa la saba, kidato cha ne na sita wa shule za Serikali imefutwa.

“Wanaotakiwa kulipa ada ya mtihani ni watahiniwa wa shule binafsi tu,” ilieleza taarifa hiyo.

Ada ya mitihani kwa darasa la saba ni Sh10,000, kidato cha nne Sh 50,000 na kidato cha sita Sh 50,000.

Siku hiyohiyo, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Twitter aliweka picha ya wanaufunzi wakiwa darasani na kuandika, “tunaendelea kutekeleza mpango wa elimu bila malipo kwa kufuta ada ya mitihani ya kidato cha nne na sita.

“Ahueni kwa watahiniwa zaidi ya 300,000 mwaka, wengi toka familia zenye kipato kidogo. Hii inakwenda sambamba na ujenzi wa shule zaidi, maboresho ya mtaala na maslahi ya walimu wetu.”

Hata hivyo, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi aliweka tangazo hilo la Necta na kuibuka mjadala uliohusisha watu mbalimbali.

“Mnatufundisha nini kwa ubaguzi huu? Hawa watoto kesho na keshokutwa watatumikia Marekani, China, Zambia au Tanzania? Nao wakianza kuitumikia nchi wabague,” alihoji Askofu Niwemugizi.

Getruda Adolfu, alijibu ujumbe huo akisema, “nimeshtuka kwa hili tangazo jamani! Baba kuna siku tutakua nchi isiyojulikana.” Huku Enock Mponzi akisema, “mmi wanangu hawajawahi kupata mkopo wa vyuo vikuu kisa walisoma shule za binafsi.”

Respicius Raymund, alisema “wazazi tunajinyima kwa ajili ya watoto wetu, tunapunguza mrundikano kwenye shule za umma na watoto wapate elimu iliyobora kwanini Serikali isilione hili.’’

Rusimbiya Ntare, yeye anadhani Serikali inatambua shule za binafsi zinasaidia kutoa elimu kwa umma, hivyo ilitakiwa kuwa mstari wa mbele kusaidia, ili lengo la kuelimisha jamii litimie lakini hapa ni kinyume.

“Serikali inaona shule binafsi kama mshindani wa kibiashara na kutafuta kukandamiza au kutoa ada za mitihani kwa shule hizi inakuwa ni kitu cha kushangaza sana,’’ alisema Ntare.

Baada ya mjadala kuendelea, Askofu Niwemugizi aliandika tena, “kodi tulipe sote ila wanufaika ni baadhi tu ya Watanzania kwa ubaguzi. Hii siyo sawa!!

Mwingine aliyechangia hoja hiyo ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Benson Bagonza aliyetoa maoni yake akisema, “huu ni upendeleo, ubaguzi, uonevu au yote matatu.”

“Shule za makanisa sio binafsi ila si za Serikali, kwanini ubia kati ya sekta binafsi na Serikali (PPP) ulianzishwa ikiwa maamuzi haya yanaweza kutolewa na Serikali.’’

Mwananchi lilipozungumza kwa simu na Askofu Bagonza alisema, “mimi nina malalamiko ya muda mrefu, kanisa unapoliweka katika kundi binafsi, ukiangalia hulikuti sehemu yoyote, kanisa na misikiti ni mali ya umma na ni makosa kuiweka katika sekta binafsi.”

“Serikali iheshimu mkataba wake wa PPP, shule za mashirika ya dini si binafsi, zinaelimisha na kutoa huduma kwa wananchi,” aliongeza

Kwa upande wake, Benjamin Nkonya, Mwenyekiti wa Jukwaa la Sera- Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) alisema tangazo hilo ni la kibaguzi.

“Shule binafsi inatoa elimu bora, kama inapigwa vita hakuna maendeleo ya kiuchumi tutaendelea kuporomoka, hawa wanaosoma na kupata elimu nzuri kwenye shule binafsi wangeweza kusaidia katika kuandaa mikataba, kuvumbua viwanda, tungekuwa tunauza bidhaa badala ya kununua,” alisema Nkonya.

Nkonya ambaye pia ni mtendaji mkuu wa Taasisi ya ubunifu katika elimu Tanzania (EIT) alisema ni suala baya kwa jamii, kwani linaongeza gharama za uendeshaji wa shule.

Alisema wanafunzi watakaokuja kwenye shule binafsi watakuwa wachache na itasababisha kuongeza ada na wanafunzi watakwenda kwenye hizo shule ambazo wanamaliza hata kuandika insha hawawezi, hivyo tutakuwa na wasomi wengi ambao hawawezi kuajiriwa.

Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo alisema walichofanya Serikali ni ubaguzi kwa asilimia 100, kwani wanaosoma shule za binafsi si wakenya wala wachina ni Watanzania ambao wana haki kama wengine.

“Shule binafsi zinasaidia Serikali, kwani haina uwezo wa kusomesha watoto wote, hawana uwezo wa kujenga shule kila mahali,” alisema Lyimo aliyewahi kuwa waziri kivuli wa elimu

Hata hivyo, alisema mitihani inatungwa na Necta na si binafsi kwa maana hiyo walitakiwa kuwaondolea wote ada ya mitihani.

Alisema wazazi wanaolipa hizo ada nao ni Watanzania na wanalipa kodi ni jukumu la Serikali ilitakiwa kuwasaidia wazazi hao wanaosemesha watoto shule binafsi, kwani hawajaweka vigezo vya kuwaondolea hawa wa Serikali hiyo ada.

Anachokisema Lyimo kinafanana na Ali Makame wa Taasisi inayojishughulisha na Makuzi na uendelezaji elimu Zanzibar (ZEWM) aliyesema Serikali inapotunga sheria au kuamua jambo linalolenga maslahi ya Taifa, lazima liwe katika sura ya kutenda haki.

“Unapotunga sheria mara nyingi unatakiwa ifanye haki kwa pande zote, sasa tukiangalia katika hili la elimu anayestahili kupata ni mtoto hata kama ni mtu mzima ina maana unajenga Taifa lenye umoja.

“Unaposema wanaosomesha shule serikalini hawatalipia ada ya mtihani, lakini wanaosoma za binafsi wanalipa ada ya mtihani ilikuwa lazima itoe ufafanuzi kwa nini,” alisema.

Othman Idd Sultan, mdau wa elimu visiwani Zanzibar alisema, “hiyo ni dalili moja ya kuonyesha tunakwenda kwenye tawala za kibaguzi na ni tawala moja mbaya sana.”

Alisema si kila mtu anayempeleka mtoto wake shule hizo ana fedha nyingi, bali wengine wanakwenda ama kwa kukosa nafasi na wengine wanaona usomeshaji wa shule za Serikali ni dhaifu.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Khadija Mussa aliyesema kama kuna tabaka ya wenye nacho na wasiokuwa nacho ni kulipeleka taifa pabaya

“Ile mitihani ni ya Taifa, kwa hiyo ni mitihani ya Serikali na ukisema wengine walipie na wengine wasilipie hiyo inaenda ndivyo sivyo na Serikali ina njia nyingi za kupata fedha,” alisema.