Wajackoyah aibukia kwa Odinga

Saturday August 06 2022
kampeni pic
By Salehe Mohamed

Hatimaye mgombea urais kupitia chama cha Roots, George Wajackoyah ameshiriki kwenye Mkutano wa kufunga kampeni wa mgombea wa Azimio la Umoja, Raila Odinga zilizofanyika katika uwanja wa Kasarani.
Hatua hii ya leo, Jumamosi Agosti 6, 2022 ya Wajackoyah inahitimisha tetesi zilizosikika siku chache zilizopita kuwa ameonyesha nia ya kumuunga mkono Odinga
Profesa Wajackoyah wiki iliyopita alinaswa kwenye video akiwa kwenye klabu ya usiku huko Kisumu akimnadi na kumsifia mgombea Raila Odinga na kuzua mvurugano ndani ya kambi yao ya kampeni huku mgombea mwenza, Justina Wamae akikana kama walikubaliana kumnadi mgombea mwingine na akionyesha bado wana nia ya kushinda urais wa nchi hiyo.
“Ni kweli kuna madai kwamba mkuu wangu na kiongozi wa chama anamuunga mkono mgombeaji wa Azimio la Umoja, lakini hatujajadili hilo kama chama, hatujakubaliana wala mimi sijashirikishwa kwenye hilo,” amesema Wamae alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari.
Wakati Wajackoyah akijipambanua kuwa upande wa Raila Odinga, mgombea mwenza wake kupitia chama cha Roots anaweza kuibukia upande wa kambi ya Naibu Rais, William Ruto, kutokana na kauli zake alizozitoa wiki iliyopita akiwa anazungumza na waandishi wa habari.
“Ikiwa msukumo unakuja na tunahitaji kuchukua msimamo juu ya nani wa kuunga mkono, kati ya wagombea wengine watatu wa urais ambao ni washindani wetu wanaostahili, basi nitaunga mkono kinyume chake (Ruto),” aliongeza.
Kitendo cha Wajackoyah kumuunga mkono Raila Odinga hakijaanza leo, hata akiwa kwenye kampeni Nyanza Juni 27, Wajackoya alifichua kwamba alifanya kazi na baba ake Odinga, aliyekuwa Makamu wa Rais marehemu Oginga Odinga na kwamba hatajali kufanya kazi na mtoto ambaye anawania urais kwa mara ya tano.
Hata hivyo, msemaji wa chama cha Roots alisema anajua mgombea wao anaweza kufanya kampeni popote na akakanusha kuwa Wajackoyah hawezi kuwepo katika uwanja wa Kasarani, ingawa yeye hayuko kwenye eneo hilo.

Advertisement