Wajackoyah, Wahiga watinga Bomas

Muktasari:

Wagombea urais, George Wajackoyah kutoka Chama cha Roots na David Waihiga leo, Jumatatu Agosti 15, 2022 wameingia katika ukumbi wa Bomas unaotumiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) ya Kenya kuhakikisha matokeo ya urais.

Nairobi. Wagombea urais, George Wajackoyah kutoka Chama cha Roots na David Waihiga leo, Jumatatu Agosti 15, 2022 wameingia katika ukumbi wa Bomas unaotumiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) ya Kenya na kuhakikisha matokeo ya urais.
Uchaguzi wa Kenya ulifanyika Agosti 9, 2022 na mpaka jana matokeo yaliyokuwa yakitangazwa kwenye vyombo vya habari yalionyesha mgombea wa Kenya Kwanza, William Ruto alikuwa akiongoza kwa kupata kura milioni 6.7 akifuatiwa na Raila Odinga wa Azimio Kwanza huku Wajackoyah akishika nafasi ya tatu na Waihiga akishika mkia.
Juzi Waihiga alitangaza kushindwa uchaguzi na kutaka IEBC imtangaza Ruto kuwa mshindi kutoka na matokeo ya kura yalivyokuwa.
Hata hivyo Wajackoyah yeye alitoa taarifa kuwa anaamini atashinda katika uchaguzi ulio huru, haki na wazi na ataendelea kusubiri matokeo ya mwisho yatakayotangazwa na IEBC.
Hata hivyo wawili hawa leo wameingia pamoja katika ukumbi wa Bomas huku wakiwa wameshika mikono ambapo walisalimia watu waliokuwa ndani ya ukumbi kisha kukumbatiana kama ishara ya upendo.
Huku wakiwa na nyuso za furaha wagombea hao walikuwa wakishangiliwa na baadhi ya watu waliohudhuria kwenye ukumbi huo na baada ya kuelekezwa sehemu ya kukaa walikwenda kwenye eneo hilo lililotengwa kwa wagombea hao.