Wajawazito wahimizwa kupata chanjo Uviko 19

Kisa wajawazito kukwama kupimwa Uviko-1

Muktasari:

  • Mganga mkuu wa manispaa ya Iringa, Dk Jesca Lebba amewataka wajawazito na wanaonyonyesha kupata chanjo ya Uviko-19 ili kuimarisha kinga za mwili za mama na mtoto.


Iringa. Mganga mkuu wa manispaa ya Iringa, Dk Jesca Lebba amewataka wajawazito na wanaonyonyesha kupata chanjo ya Uviko-19 ili kuimarisha kinga za mwili za mama na mtoto.

Amesema hayo wakati wa kuhamasisha wananchi wa manispaa ya Iringa kupata chanjo ya Uviko kupitia mpango wa jamii shirikishi na harakishi unaoendeshwa na Wizara ya Afya, Tamisemi na wadau wa sekta ya afya.

Amewatoa hofu wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na makundi mengine katika jamii kuhusu chanjo ya Uviko-19 akiwataka kutoogopa  kupata chanjo kwa kuhofia kiumbe aliyepo tumboni pamoja na maziwa ya mtoto.

“Nawahimiza akina mama wote wajitokeze kwa ajili ya kuchanja kwa kuwa chanjo hii ni salama na haina madhara yoyote kwa mama mjamzito wala anayenyonyesha. Mjamzito  anapokuwa ananyonyesha kinga ya mwili zina tabia ya kushuka kutokana na mahitaji ya mwili kuongezeka, kwa hiyo ni vyema mkapata chanjo ili kujikinga na Uviko-19  ” amesema Dk  Lebba.

Magdalena Thobias ambaye ni mjamzito amesema awali alikuwa anaogopa kwenda kupata chanjo kwa kuwa alihofia maisha yake na ya mwanaye.

"Kwa sasa nimepata elimu hii ya chanjo na madaktali wametushauri kupata chanjo ya Uviko-19 ni bora zaidi kuliko kutopata kwa sababu sisi wajawazito muda mwingi tunakuwa dhaifu ,kupata chanjo hii kutanihakikishia usalama wangu na wa mtoto wangu aliye tumboni," amesema Magdalena

Kwa upande wake Juma Hassan Mkazi wa Iringa amewashukuru wataalam wa afya kwa kupita mtaa kwa mtaa kuwajengea uwezo juu ya chanjo ya Uviko 19 kwani watu wengi hawana uelewa juu ya chanjo na wengine hawana sababu ya msingi ya kukwepa chanjo  wala namna sahihi ya kujikinga.

"Tunashukuru madaktari  wanapita mitaani kutupa elimu ya chanjo watu wengi wanaogopa kupata chanjo na wengine wanakwepa bila sababu ya msingi jambo hili linatufanya tuwe hatarini kupata maambukizi ya Uviko na tumejifunza usipopata chanjo ukipata maambukizi unakuwa hatarini zaidi,hivyo ni vyema kila mtu akapata chanjo," amesema