Wakala wa ushuru atupwa jela miezi 60

Muktasari:

  • Mahakama  ya Wilaya ya Kilwa,Mkoani Lindi,imemtia hatiani Wakala wa kukusanya ushuru katika Halmashauri hiyo, Darasa Ally Mwamba (40) na kumpa adhabu ya kutumikia kifungo cha miezi 60 jela na kurejesha fedha alizoiba alipokuwa akitekeleza majukumu aliyokabidhiwa.

Lindi. Mahakama  ya Wilaya ya Kilwa,Mkoani Lindi imemtia hatiani Wakala wa kukusanya ushuru katika Halmashauri hiyo, Darasa Ally Mwamba (40) na kumpa adhabu ya kutumikia kifungo cha miezi 60 jela na kurejesha fedha alizoiba alipokuwa akitekeleza majukumu aliyokabidhiwa.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Alisi Kasera baada ya mshtakiwa kukiri kosa linalomkabili.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshitakiwa alijitetea kwa kuiomba mahakama isimpe adhabu kali kwakuwa ni mara ya kwanza kufanya kosa hilo na anajutia kosa alilolifanya, ana familia inayomtegemea na anaye mgonjwa anayeesumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa moyo.

Baada ya utetezi huo, Hakimu Kasera alimuuliza Mwanasheria wa Takukuru iwapo anazo kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshtakiwa na alijibu hana lakini aliiomba Mahakama impatie adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.


Hakimu Kasera alisema kwa kosa la kwanza la matumizi mabaya ya mamlaka mtuhumiwa atapaswa kulipa faini ya Sh1 milioni akishindwa aende Jela miezi 12.

Kosa la pili kugushi nyaraka za fedha kifungo cha nje miezi 24 kosa la tatu la wizi wa fedha za umma atatumikia kifungo cha nje miezi 24 na kufanya kifungo chote kuwa cha miezi 60 sambamba na kurejesha Sh3 milioni alizoiba.

 Awalii ilidaiwa Mahakamani hapo na mwanasheria wa taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru ) Mkoa wa Lindi, Osborn Mulamula, alidai mshitakiwa alifanya makosa hayo kati ya Januari 2013 na Oktoba 2015 alipokuwa anakusanya ushuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.