Wakandarasi waliosajiliwa CRB wafika zaidi ya 14, 000

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa CRB wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi unaofanyika jijini Mwanza wakifuatilia mada. Picha na Saada Amir

Muktasari:

Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) imesajili wakandarasi wapya 1,341 mwaka 2022 na hivyo kufanya idadi ya wakandarasi waliosajiliwa nchini Tanzania kufikia 14,034.

Mwanza. Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) imesajili wakandarasi wapya 1,341 kwa mwaka 2022 na kufanya idadi ya wakandarasi waliosajiliwa kufikia 14,034 nchini.

Akizungumza kwenye mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi uliofanyika leo Alhamisi 30, 2023 jijini Mwanza, Msajili wa CRB, Mhandisi Rhoben Nkori amesema bodi hiyo pia iliwafutia usajili wakandarasi 520 baada ya kufanya tathimini ya wakandarasi wote iliyowasajili na kugundua baadhi yao kukosa sifa na wengine kuachana na fani hiyo kutokana na suala la ‘force account’

“Suala la force account lilikuwa linaleta shida na kero kubwa kwa wakandarasi na hata tulivyosema 520 tumewafutia usajili wengi walibadilisha biashara kwa sababu walikuwa hawana kazi za kufanya lakini tumeanza kuona ongezeko la kazi za majengo ya Serikali na taasisi zake zikitolewa kwa makandarasi na tunaamini Serikali itaendelea kuongeza matumizi ya huduma za makandarasi katika kazi zake nyingi,”amesema

Licha ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha wakandarasi hususan changamoto ya upungufu wa kazi kwa makandarasi wa majengo kutokana na suala la force account, Nkori ameikumbusha Serikali kuangalia upya sheria ya manunuzi ya umma pamoja na kanuni zake katika eneo la dhamana za zabuni na dhamana za utekelezaji akidai kwa mujibu washeria hiyo mwajiri ndiye amepewa uwezo wa kuamua aina ya dhamana itakayotumika ambayo ni lazima itumike kwa wazabuni wote .

“Uzoefu umetuonesha waajiri wengi huchagua matumizi ya dhamana za benki na wakishaamua hivyo lazima wazabuni wote wa mradi huo wapeleke dhamana za benki hapa pia naomba niipongeze Serikli kwa kuweka utaratibu wa dhamana za kiapo hata hivyo kwakuwa matumizi hayo ni kwa miradi midogo na ya kati pekee, tunaomba iruhusiwe kwa miradi ya hadi Sh10 bilioni,”amesema

Ameomba waajiri waangalie matumizi ya dhamana ya bima hata kwa miradi mikubwa ili kuwawezesha makandarasi wengi zaidi kushiriki katika zabuni na utekelezaji wa miradi mikubwa, watatue changamoto ya ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi, waongeze malipo ya awali kutoka asilimia 15 ya sasa hadi 25 kutokana na mahitaji halisi ya mradi, ziada ya kodi ya zuio ambayo inafanyika kwa wakandarasi itumike kulipia kodi zingine au kuirejesha kwa mkandarasi na si kuendelea kuizuia kama ambavyo inafanyika pamoja na waajiri kubeba gharama za tozo za vifaa vya ujenzi.

Katika kikao hicho chenye lengo la kuwakutanisha kwa ajili ya kupeana taarifa, kushauriana, kujithamini, kujisahihisha na kuweka mikakati madhubuti kuboresha ufanisi katika shughuli za ujenzi nchini, Nkori amesema mwaka jana CRB ilisajili miradi 4,013 yenye thamani ya Sh6.128 trilioni ambapo asilimia 50.1 ilifanywa na wakandarasi wa ndani na asilimia 49.9 ilitekelezwa na wakandarasi wageni.

“Bodi ilikagua miradi 3,728 ambapo miradi 2,494 ambayo ni asilimia 67 haikuwa na kasoro na miradi 1,236 sawa na asilimia 33 ilikuwa na kasoro mbalimbali ambapo bodi ilitoa maelekezo stahiki kwa mujibu wa sheria kwa miradi iliyokutwa na kasoro,”amesema

Akifungua makutano huo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Godfrey Kasekenya amesema matumizi ya force account yataendele kupungua huku akiitaka bodi hiyo kuongeza bidii kusajili, kudhibiti na kuendeleza makandarasi.

“Kuhusu changamoto ya kuchelewa malipo ya makandarasi, napenda mfahamu kuwa ni nia thabiti ya Serikali kuona makandarasi wanalipwa kwa wakati, Serikali itaendelea kufanya jitihada kuhakikisha malipo kwa makandarasi yanalipwa kwa wakati,

“Kwa sababu ucheleweshaji huo huathiri makandarasi, Serikali na wananchi kwa ujumla kwa kutokamilika kwa miradi husika kwa wakati hivyo wananchi kuchelewa kupata huduma iliyokusudiwa,”amesema

Akijibu ombi la makandarasi kuiomba Serikali kuchukua hatua za makusudi kuweka mfumo wa kuhakikisha wataalam wa ngazi za kati katika fani mbalimbali za ujenzi wananaboreshewa miundombinu ya mafunzo kwa vitendo, Kasekenya ameagiza kuanzishwa programu za kupokea wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo huku akiahidi kufanyia kazi changamoto zingine zilizowasilishwa kwenye makutano huo.