Wakazi Butiama watembea kilomita 30 kufuata huduma za afya

Meneja wa Benki ya Biashara ( TCB), Hagai Gilbert (kulia) akimkabidhi diwani wa kata ya Hunyari, Mugungi Muhochi ( anayefuata) sehemu ya mabati ambayo benki hiyo imetoa kwa ajili ya kusaidia katika ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Nyamikoma wilayani Butiama ambapo benki hiyo imetoa msaada wa mabati 135 yenye thamani ya zaidi ya Sh5 milioni.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Wakazi wa kijiji cha Nyamikoma wilayani Butiama wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 30 kutafuta huduma za afya hali ambayo imesababisha benki ya biashra kutoa msaada wa mabati yenye thamani ya sh5 milioni kwaajili ya mradi wa ujenzi wa zahanati kijijini hapo.

Butiama. Wakazi wa kijiji cha Nyamikoma kata ya Hunyari wilayani Butiama, Mkoa wa Mara wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 30 kutafuta huduma za afya.

Hali hiyo inatokana na kijiji hicho kutokuwa na zahanati kama inavyoelekeza sera ya afya hatua mabayo imekuwa ikisababisha kero mbalimbali ikiwemo wanawake wajawazito kujifungulia njiani kabla ya kufika kwenye kituo cha afya katika kata ya jirani.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Machi 19, 2023 na diwani wa hiyo, Mugungi Muhochi wakati wa kupokea masada wa mabati kutoka Benki ya Bishara Nchini (TCB).

Amesema kuwa kutokana na adha hizo wakazi wa kijiji hicho kwa pamoja waliamua kuanzisha ujenzi wa zahanati ili kuweza kupata suluhisho la kudumu juu ya chagamoto hizo.

"Hadi sasa wamejenga jengo na kufikia hatua ya upauaji sasa wanaomba msada kwa wadau mbalimbali waweze kusaidia ukamilishaji wa boma hili ili hatua zingine ziendelee kubwa zaidi ni huduma kuanza kutolewa," amesema

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Adam Tobi amesema Sh150 milioni zinahitajika ili kukamilisha jengo la zahanati kijijini hapo.

"Hadi sasa tumetumia Sh57 milioni hadi kufikia hapo jengo lilipo ambapo wakazi wa kijiji changu wametoa Sh17 milioni na Sh40 milioni zimetolewa na wadau mbalimbali," amesema

Ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kusaida ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati hiyo ambayo amesema kuwa ni hitaji kubwa la wakazi 9,000 wa kijiji hicho na maeneo jirani.

Meneja wa TCB tawi la Musoma, Hagai Gilbert amesema benki yake imetoa msaada wa mabati 135 yenye thamani ya zaidi ya Sh5 milioni kama mchango wa kufanikisha ujenzi huo.

Amesema msaada huo ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) na kwamba suala la afya ni suala muhimu katika maendeleo kwa ujumla.

"Serikali pekee haiwezi kukamilisha kila kitu, tumeona na sisi tuunge mkono jitihada za serikali na wananchi hawa lakini pia  na sisi ili biashara yetu iweze kufanikiwa tunahitaji watu wenye afya bora na afya bora inapatikana pale ambapo huduma za matibabu zinapopatikana kwa uhakika na ukaribu zaidi," amesema Gilbert.

Mkazi wa kijiji hicho, Anastazia John amesema kuwa kutokana na changamoto wanazokumbana nazo wakati wa kutafuta huduma za afya wanatamani jengo hilo likamilke haraka na kuanza kutoa huduma mara moja.

"Hebu fikiria yule anayeuguliwa au kuugua usiku wa manane jinsi anavyohangaika kupata usafiri hadi kufika kituo cha afya, akinamama uchungu huwa hauna muda maalum ukianza kuuma usiku mwisho wake tunaishia kuzalia njiani tunaomba wadau watuunge mkono," amesema