Wakili Basila: Tatizo kubwa Tanzania ni uzalendo

Wakili Moses Basila akizungumza na baadhi ya wananchiwa Kijiji cha Njoro Kiteto ambao wanachangamoto ya migogoro ya ardhi ambayo imechangiwa na baadhi ya viongozi kuwawajibika katika nafasi zao Kikamilifu. Picha na Mohamed Hamad

Kiteto. Wakili Moses Basila amesema kiwango cha uzalendo kwa baadhi ya viongozi ni kidogo hali inayochangia wananchi kuwa na changamoto katika huduma.

 Basila ameyasema hayo leo Februari 15, 2023 mjini Kibaya kuwa changamoto nyingi zinazowakumba wananchi ni kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali kuwa na kiwango kidogo cha uzalendo katika kutumikia nafasi walizoaminiwa na wananchi.

Amesema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema moja ya mambo muhimu kwa nchi hii ni pamoja na uongozi bora.

“Haya mengine acha nianze na eneo hilo la uzalendo ukikosekana huwezi kupata ladha ya uongozi bora na matunda kumwendea mwananchi kwa maslahi ya nchi kwa ujumla...kwa hiyo tatizo kubwa hapa Tanzania ni uzalendo," amesema Basila.

Amesema chuo cha uongozi kina kazi kubwa ya kufanya na hata kile cha Mwalimu Nyerere Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma na wana kazi kubwa ya kufanya, haki za binadamu na utawala bora, Tume ya Utumishi wa Mahakama na wananchi wenyewe wana wajibu kuhakikisha tunatoka hapa tulipo kama Taifa.

Huu uzalendo unaanzia kwa mwananchi wa chini na viongozi. Tatizo la pili ni sheria ya kumwajibisha aliyeaminiwa na Serikali na ana wajibu wa kuwatumikia wananchi ambaye anaathiri ustawi wao ama maendeleo ya Taifa. Amesema ni sheria gani ziwepo kukabiliana nao?

Amesema kuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, matokeo yake ya kiutendaji  inampa wasiwasi kwani kuna changamoto kubwa zinaendelea kujitokeza Serikali za mitaa lakini haoni zikishughulikiwa kikamilifu. "Uwajibikaji wa hizi taasisi ni wa maslahi ama umma au nchi, nina maswali mengi…Kuna shida kwenye sheria zetu ama ni uzalendo? Wakati mwingine najaribu kuja na hoja ya katiba hoja ambayo sipendi kuizungumzia nina maslahi nayo binafsi, lakini ukatiba unahitajika ili udhibiti haya ili kupata uzalendo unaoweza kuacha matokeo Tanzania,"alisema Wakili Basila.

Amesema ukatiba wa zamani ukitumika kudhibiti ukatiba wa sasa kutakuwa na hoja ambazo zitakosa majibu. Najiuliza pia kama sheria zilizopo zinaathiri uzalendo zikija sheria zingine mpya zitabadilisha uzalendo wa wananchi? Ni muda sahihi wa kuzitamani hizo?

Hata kama ni muda sahihi ni sasa? Ni maswali ambayo bado yanahitaji utafiti…Siwezi kusema tu kwa pamoja tatizo ni la katiba pale ambako kuna uwajibikaji mbovu sheria iliyonyooka kabisa ikavunjwa na mvunjaji asione madhara ya kufanya hivyo ni tatizo," amesema.

Kwa upande wake, Thomas Njama amesema kuna baadhi ya watumishi wa Serikali kwa utashi wao wa kutumia mamlaka waliyonayo wamekuwa wakifanya maamuzi ya kuathiri wananchi na wala hawahojiwi huku wananchi wakiendelea kuathirika.

Abasi Famau mwangalizi wa haki za binadamu Kiteto, amesema jamii bado inauelewa mdogo wa masuala ya sharia, kazi kubwa inayotakiwa kufanyika kwanza wajue wajibu wao wajibu wa viongozi na sheria mbalimbali.