Wakili kesi ya Zumaridi aomba kupumzika kabla ya kumhoji shahidi

Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi akiwa ndani ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza. Zumaridi na wenzake nane wanakabiliwa na kesi namba 10/2022 yenye makosa kushambulia maofisa wa umma na kuwazuia kutekeleza majukumu yao. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Zumaridi na wenzake nane wanashtakiwa kwa makosa ya kufanya shambulio dhidi ya maofisa wa umma na kuzuia maofisa wa Umma kutekeleza majukumu yao.

Mwanza. Wakili katika Kesi ya Jinai namba 10/2022 inayomkabili Diana Edward maarufu kama Mfalme Zumaridi na wenzake wanane, Erick Mutta ameiomba mahakama kusimama kwa dakika 15 ili apumzike kabla hajaanza kumuuliza maswali shahidi wa sita.

Zumaridi na wenzake wanane wanashtakiwa kwa makosa ya kufanya shambulio dhidi ya maofisa wa umma na kuwazuia maofisa wa Umma kutekeleza majukumu yao.

Leo Agosti 10, kabla ya shahidi huyo ambaye ni ofisa wa Polisi mwenye namba F1468 Sajenti Johaness Mlashani kuanza kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo, alitanguliwa na Ofisa mwenzake wa jeshi la Polisi, WP4592 Sajenti Paulina.

Ilipofikasaa 6:14 mchana, Sajenti Mlashani aliitwa ndani ya chumba cha mahakama na kuanza kutoa ushahidi kisha kusoma maelezo aliyochukua kutoka kwa mshtakiwa namba moja ambaye ni Mfalme Zumaridi.

Kwenye ushahidi wake, Sajenti Mlashani amesema baada ya kumchukua Zumaridi alimpeleka katika Ofisi yake kisha kubaki naye na kuanza kumchukua maelezo.

Ameieleza mahakama hiyo kwamba kabla ya kuanza kuchukua maelezo alimsomea mtuhumiwa (Zumaridi) baadhi ya haki zake za msingi ikiwemo kujitambulisha kwake, kumtaka mtuhumiwa aite ndugu, jamaa au rafiki ili awepo wakati wa kuchukuliwa maelezo yake jambo ambalo Zumaridi alidai haoni haja kwani anamwamini Mungu wake.

Hata hivyo, baada ya kufanya hivyo Mlashani amesema alimuuliza Zumaridi iwapo anajua kusoma na kuandika ndipo Zumaridi alipomjibu kwamba anajua kuandika japo kasi yake ni ndogo.

Amesema baada ya majibu hayo, Zumaridi alimuomba ofisa huyo aandike maelezo anayotoa huku akiahidi kuyapitia watakapomaliza kisha kuwela saini iwapo ataridhishwa nayo jambo ambalo alilifanya baada ya mahojiano kumalizika.

Shahidi huyo amesema baada ya kumaliza kuandika maelezo ya mshtakiwa huyo aliwayawasilisha kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali ambaye aliamua kufungua mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Monica Ndyekobora akatoa nafasi kwa jopo la mawakili wa utetezi kumuuliza shahidi maswali, ndipo Wakili wa Utetezi, Erick Mutta alipoomba dakika 15 za mapumziko kabla kuanza kumuuliza maswali.

Dakika 15 zakamilika

Ilipofika Saa 6: 30 Wakili, Mutta alianza kwa kumuuliza shahidi na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo;

Wakili Mutta: Shahidi tusaidie kutueleza kwenye kesi iliyopo mbele ya mahakama jukumu lako lilikuwa ni nini?

Shihidi: Kupeleleza, kuandika maelezo na kutoa ushahidi


Wakili Mutta: Kuna mpelelezi mwingine tofauti wewe?

Shahidi: Hakuna mpelelezi mwingine

Wakili Mutta: Unakubaliana na mimi kwamba upelelezi ni jambo la kisayansi.

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili Mutta: Linaloongozwa kwa misingi ya kisheria?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili Mutta: Baada ya kuandika maelezo ya washtakiwa wawili uliyowaeleza unasema uliandika na maelezo ya mhanga wa tukio?

Shahidi: Hapana, aliandika yeye mwenyewe

Wakili Mutta: Je alikupatia ukayasoma?

Shahidi: Baada ya kuyaandika alinipatia nikayasoma

Wakili Mutta: Kuna shahidi mwingine ulimwandika maelezo?

Shahidi: Walinipa na askari wengine.

Wakili Mutta: Ila maelezo hayo ulipewa vile vile ukayasoma?

Shahidi: Niliyasoma ambao ni Afisa Ustawi wa Jamii na Inspekta Paulo nilisoma maelezo yao.

Wakili Mutta: Unakubaliana na mimi mpelelezi ndiye anayesona na kugundua ushahidi umekidhi kuanzisha mashtaka?

Shahidi: Mpelelezi wa kesi ndiyo anayeandikia faili kwenda ofisi ya mashtaka baada ya kuona ushahidi umekidhi kuanzisha mastaka.

Wakili Mutta: Wewe kama mpelelezi kwenye jalada ukakuta maelezo ya mashahidi yanapishana unatakiwa kufanya nini?

Shahidi; Ninachokifanya ni kuliandikia jalada kwenda ofisi ya mashtaka kwa ajili ya kusoma mashahidi yaliyomo ndani ya jalada endapo wakibaini ushahidi huo unaweza ukamuweka mshkatiwa hatiani basi wanafungua kesi.

Baada ya wakili wa utetezi kumaliza maswali yake, Hakimu Mkazi Mwandamizi aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 18 mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa shahidi wa saba katika shauri hilo.