Wakulima wa Korosho walalamikia kushuka kwa bei

Muktasari:

  • Wakulima wa zao la Korosho Wilayani Newala na Tandahimba  wamesikitishwa na kushuka kwa bei za korosho huku barua sita tu zikifika mnadani ikitofautiana na mnada wa 10 ambao barua 16 ziliweza kuwasilishwa mnadani hapo.

Mtwara. Wakulima wa zao la Korosho Wilayani Newala na Tandahimba  wamesikitishwa na kushuka kwa bei za korosho huku barua sita tu zikifika mnadani ikitofautiana na mnada wa 10 ambao barua 16 ziliweza kuwasilishwa mnadani hapo.

Awali katika mnada huo bei ya juu ilikuwa ni Sh1,852 huku bei ya chini ikiwa ni Sh1,700 ambapo zaidi ya tani 2800 ziliuzwa huku mnada uliopita wa 10 zikiuzwa tani 3500.

Akizungumza katika Mnada wa 11 uliondeshwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba &Newala  (Tanecu),  Mahamood Baraza mkulima wa korosho kutoka kijiji cha Mtopwa amesema kuwa amelazimika kuuza korosho hizo japo hapati faida yoyote kutokana na bei kuzidi kushuka.

Alisema kuwa mkulima anatumia fedha nyingi kuandaa shamba kupuliza dawa kwa gharama kubwa hivyo kuiomba serikali iliangalie bei hizo kwa minada ijayo iweze kurekebisha.

"Mimi nimelidhia kuuza korosho sio kwamba nimeridhishwa na bei hapana bei hainifurahishi na wala hainisaidii lakini nisipouza zikarudi nyumbani itanisaidia nini tunalazimika kuuza laiti tungekuwa na namna nyingine tungeweza kukataa kuuza haitasaidia kitu"

Nae Diwani wa kata ya Mtopwa, Mohamed  Yusuph alisema kuwa  bei ya korosho inazidi kushuka hali ambayo ina muumiza mkulima wa zao hilo.


"Kwaweli bei inazidi kushuka hatujui sababu lakini hairidhishi hatuoni kama ni haki  wakulima wanafanyakazi kubwa sana shambani tunapaswa kuwaangalia ili waweze kuuza korosho kwa bei zenye tija" alisema Yusuph

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya chama kikuu cha ushirika TANECU Karim Chipola alisema kuwa bei sio rafiki kwa mkulima na hafurahishwi nazo.

"Korosho zina gharama hadi kufikia kwa mkulima hizi bei sio rafiki angalia kuanzia mkulima anapoandaa shamba upuliziaji vyote anatumia vibarua zikianza kudondoka anatumia vibarua pia kuokota hii sio sawa yaani wameuza ili mradi tu wanunuzi waangalie hili waongeze bei" alisema Chipola