Wakulima wa mahindi waiomba serikali kuiongezea NFRA fedha

Muktasari:

  • Wakulima wa mahindi mkoani Njombe wameiomba serikali kuiongezea fedha Wakala wa wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Makambako ili iweze kununua mahindi ambayo bado yapo kwa wakulima.

Njombe. Wakulima wa mahindi mkoani Njombe wameiomba serikali kuiongezea fedha Wakala wa wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Makambako ili iweze kununua mahindi ambayo bado yapo kwa wakulima.

Kauli hiyo wameitoa leo Oktoba 18 ikiwa ni siku chache baada ya NFRA kanda ya Makambako kuhitimisha ununzi wa mahindi kwa wakulima yenye thamani ya Sh5 bilioni zilizotolewa na serikali kwenye kanda hiyo.

Wamesema utaratibu uliotumika katika kuuza mahindi kwa NFRA kanda ya Makambako ulikuwa mzuri lakini bado wana kiasi kikubwa cha mahindi hivyo wanaiomba serikali kuongeza fedha ili waweza kuuza na kupata fedha za pembejeo.

Wamesema utaratibu ulifuatwa, ambapo vyama vya ushirika viliweza kuuza mahindi ambapo pia mkulima mmoja mmoja aliweza kuuza mahindi yao.

Wamesema baada ya serikali kuweka bei ya kilo ya mahindi Sh500 kwa kilo iliwahamasisha wakulima kuuza mahindi yao.

Baadhi ya wakulima hao akiwemo Ally Lukuvi na Robert Masanja waliiomba serikali kuendelea kuwatazama wakulima kwa kuongeza bei ya mahindi ili waweze kufanya kilimo hicho ambacho kimeonyesha mafanikio kwasasa.

"Bei ilikuwa inatuathiri sana wakulima kwani mbolea tulikuwa tunanunua kwa bei kubwa lakini mahindi tunauza kwa bei ndogo," amesema Masanja.

Kwa upande wake Kaimu meneja wa NFRA kanda ya Makambako, Frank Felix amesema zaidi ya tani 10,000 zimenunuliwa kutoka kwa wakulima ambayo thamani yake ni Sh5 bilioni ikiwa ni sehemu ya fedha ambazo zilitolewa na serikali ili kununua mahindi kwa wakulima.

Amesema kanda hiyo imekuwa na misimu miwili, ikiwemo ya kwanza, ambayo NFRA inapokea bajeti kutoka serikalini, lakini waliongeza awamu ya pili ambayo zilitolewa Sh50 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa mahindi nchi nzima.

Amesema mpaka kufikia Oktoba 14 mwaka huu kanda hiyo ilikamilisha ununuzi wa tani 10,000 za mahindi.

"Mpaka sasa hivi tuna jumla ya tani 10,000 na kilo 60,000 tulizonunua kwenye vituo vyetu mbalimbali ikiwemo Makambako, Ludewa na maeneo mengine," alisema Frank.

Mkuu wa wilaya ya Njombe, Kisa Gwakisa Kasongwa amemshukuru raisi Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa NFRA kwenye kanda hiyo kwani wakulima wa mahindi  walikuwa na kilio kikubwa kutokana na bei ndogo na kukosekana kwa wanunuzi.

“Wamefanikiwa kununua mahindi kwa bei ya shilingi mia tano kwa kilo bei ambayo wakulima wameifurahia hivyo kwa niaba ya wananchi wa Njombe tunamshukuru Rais kwani wananchi wamenufaika sana zoezi hilo," alisema Kasongwa.