Wakulima wa minazi wataka wataalamu kutoka ofisi wakawasaidie

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ally (kushoto), akipokea maelezo kutoka kwa Meneja wa Kituo cha  Tari, Mikocheni jijini Dar es Salaam, Dk Fred Tairo leo Juni 11, 2024.

Muktasari:

  • Wakulima wa zao la Minazi wapaza sauti, wataka wataalamu wa kilimo kutembelea kwenye mashamba yao kuwapa mbinu za kisasa zitakazowawezesha kukabiliana na changamoto.

Pwani. Wakulima wa zao la minazi, Wilaya ya Mkuranga wamesema uhaba wa watalaamu wanaoweza kutoa mbinu za kisasa za kilimo hicho ni  sababu ya zao hilo kukosa hamasa kila uchwao hususan kwa vijana.

Wamesema hata maofisa ugani wachache waliopo katika maeneo yao wanatumia muda mwingi kushinda ofisini badala ya kuwatembelea wakulima mashambani kuwapa elimu ya kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.

Hayo wamezungumza wilayani hapo jana, kwenye siku ya Mkulima iliyoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni (Tari) ikiwa na lengo la kuhamasisha wakulima kuzingatia kilimo cha kisasa ili kupata tija.

Mkulima wa zao la minazi, Rozi Mipiko amesema miaka ya nyuma zao hilo, linasumbuliwa na magonjwa na ilifikia hatua ilikuwa inakufa  kwa kukosa utafiti wa kupata tiba ya kudhibiti.

"Hali ile ilisababisha watu wengi kukata tamaa ya kulima  kilimo hiki, kuna magonjwa yaliibuka na kupewa majina mengi kama wadudu chonga. Utitiri ilikuwa inakauka lakini watalamu hawakuonekana na hata wachache tulikuwa tunawafuata walikuwa hawana msaada," amesema.

Rozi ambaye ni mstaafu wa Serikali miaka saba iliyopita akimiliki shamba lenye heka tano, amesema  kama wataalamu wangekuwa wanatoa elimu au kufanya utafiti kwa kuwashirikisha wakulima wengi ingechochea  kuhamasika.

"Ushauri wangu  Serikali kama ina dhamira ya kurudisha nguvu zao la minazi ni muhimu wataalamu wawe karibu na wakulima mahitaji ni makubwa ikiwemo miche ya kisasa na viwatilifu," amesema Rozi.

Mkulima wa zao hilo, Said Ramadhani  amesema tatizo lingine licha ya kujitahidi kulima zao hilo lakini soko linakuwa gumu kwao na matokeo yake madalali wamekuwa wakinufaika zaidi.

"Tukiwa shambani nazi moja tunauza Sh500 kwa shida kwa wachuuzi lakini wao wanauza kwa Sh800 hadi Sh1,000. Tunaomba mtusaidie kupata soko zuri  ili bei ipande tupate fedha ya maana ili tuendeshe mashamba yetu," amesema.

Amesema kuendelea kudorora kwa bei ni sababu ya zao hilo kuyumba yumba mara kwa mara na inasababisha hata vijana wengi kukimbilia mijini kutafuta maisha na kuwaacha wazee wakiangaika.

"Wanaona zao la nazi halina maslahi unafanya kazi mwisho wa siku hadi mgongo unapinda hauna fedha ya maana, hata mikopo hatupati kabisa," amesema.

Akianza kujibu maswali hayo ya Wakulima, mgeni rasmi wa tukio Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ally amewataka wataalamu hao kutoka maofisini na kuwafuta wakulima mashambani.

"Mnatakiwa kutembea sokoni na kutoa elimu kwa wakulima badala ya kuendelea kukaa ofisini haipendezi, tambueni mnalojukumu la kuwaelimisha na kuwapa ushauri wa kitaalamu wakulima waache kulima kizamani kama mababu zetu," amesema.

Amesema zao la minazi ni moja ya mazao ya kimkakati shabaha ya serikali liwe na tija na kuongeza pato katika taifa kama ilivyo Indosia asilimia 51 ya pato lake linatokana na kilimo cha minazi.


Kuanzia bodi ya zao la nazi

Katika hatua nyingine, Meneja wa Kituo cha  Tari, Mikocheni Dar es Salaam, Dk Fred Tairo amesema Serikali kupitia Tari bado wapo kwenye mkakati wa kukusudia kuanzisha bodi ya zao hilo lengo kusimamia maslahi ya wakulima wa zao hilo.

"Tupo kwenye bodi ya mazao mchanganyiko na kinachotatiza kupata takwimu za kutosha tukijua na itasaidia kusudio la Serikali kuanzia bodi itakayokuwa inasaidia kulinda maslahi ya zao la Minazi," amesema Dk Tairo.

Dk Tairo amesema kuanzia sasa kituo hicho cha Tari Mkuranga kitakuwa wazi na kitakuwa kinatoa huduma kwa mwaka mzima na kuwataka wakulima wa zao hilo kwenda kupata ushauri na elimu.


Hali ya zao la minazi Mkuranga

Akizungumza hali ya kilimo cha minazi katika Wilaya ya Mkuranga, Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Anna Kiria amesema wilaya hiyo kupitia wakulima wake wanalima zao hilo jumla ya hekta 2,1141 na wanazalisha tani 33,278.