Wakulima wamuomba Rais Samia shamba hekta 200

Mwenyekiti wa TCCIA Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Jeny Mbago akichangia hoja wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya shughuli zao la tija yaliyoandaliwa na TCCIA Mkoa wa Pwani na kufanyika Mjini Kibaha. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Wakulima Pwani walivyowasukuma viongozi wao kufikisha changamoto zao kwa Rais ili zifanyiwe kazi kwa wakati.

Kibaha. Wakulima wa mpunga na mazao mchanganyiko  walionyang'anywa zana za kilimo na mamlaka mbalimbali kwa madai ya kuzitumia kinyume na utaratibu katika Bonde la Mto Ruvu mkoani Pwani wameuomba uongozi wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani humo kuwasaidia ili warejeshewe vifaa vyao ambavyo watavitumia kulingana na taratibu za sheria zinavyoagiza.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi yaliyoandaliwa na TCCIA na kufanyika Kibaha mkoani Pwani mmoja wa wanachama hao, Mzee Bora  amesema kuwa kutokana na hali hiyo hivi sasa wanashindwa kuendesha shughuli zao kwa ufanisi hivyo ni vyema wakarejeshewa zana zao ziwasaidie.

"Sisi mbali na kilimo pia tunajihusisha na ufugaji wa nyuki tuna kikundi chetu ili tuendeshe maisha, tunahitaji kufanya kazi kwa kuzalisha kwa tija na nyenzo kuu ni zana za kilimo, lakini tulinyang'anywa mashine za umwagiliaji na mipira hivyo inatuwia ugumu,"amesema.


Amesema kuwa wanachotamani ni kurejeshewa mashine hizo na watakaowasaidia ni viongozi wa TCCIA kwani wao wako kwenye mwamvuli wao.

Wamesema kuwa awali walivyochukuliwa zana hizo waliahidiwa kuwa wangerudishiwa, lakini takribani ni mwaka umepita mpaka sasa hawaoni dalili za kupewa vifaa hivyo ambavyo ndivyo vitendea kazi muhimu kwenye shughuli zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TCCIA, Jeny Mbago ameuomba uongozi wa chemba hiyo ngazi ya Mkoa na Taifa kuwafikishia ombi lao kwa Rais Samia Suluhu Hassan la kupatiwa shamba lenye ukubwa wa hekta 200 ili walitumie kwa kilimo cha miwa kwa kuwa soko la bidhaa hiyo ni muhimu kwa jamii.

"Jumla tuko wanachama 350 kwa halmashauri zote mbili Bagamoyo na Chalinze na kuna uhitaji wa wengine kujiunga hasa vijana wanaohitimu masomo hawana ajira, bali ajira yao ya kilimo cha miwa itawakomboa na hili ni ombi letu la muda mrefu tupate ardhi tulime miwa,"amesema.

Amesema kuwa endapo watafanikiwa kupata ardhi hiyo ambayo kwa macho wameshaiona inafaa kwa kilimo wataokoa maisha ya vijana wengi kutijiingiza kwenye kazi za hatari ikwemo wizi na mambo ya zinaa hasa kwa wasichana.

Katibu wa TCCIA Mkoa wa Pwani, Amilwise Mkayula alisema kuwa lengo la kuwapa mafunzo hayo wanachama hao ni kuwaongezea uelewa ili kutambua namna bora ya kuendesha shughuli zao kuheshimu sheria za nchi na kulipa kodi kwa hiari.

Afisa Masoko na Uhusiano kutoka UTT AMIS, Oliver Minja aliwataka wafanyabiashara hao kujiwekea utaratibu wa kutunza akiba kwa njia salama kwani zitakuwa msaada kwao pindi watakapofikia umri wa kushindwa kufanya kazi.

Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Pwani, Saidi Mfinanga ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na wanachama hao Ili zitatuliwe na kuwezesha kufanya uzalishaji kwa tija.

Awali, akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala Msaidizi Uwekezaji Viwanda na Biashara Mkoa wa Pwani, Rehema Akida amewataka wafanyabiashara hao kuheshimu sheria za nchi ikiwemo kulipa kodi zilizopo kisheria ili Serikali iendelee kuwaletea maendeleo.