Wakuu wa wilaya Simiyu wabwagwa uchaguzi CCM

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange ambaye ni mmoja wa wakuu wa wilaya mkoani Simiyu walioshindwa katika uchaguzi wa CCM ambapo alikuwa anawania nafasi ya ujumbe mkutano mkuu taifa. Picha na Samirah Yusuph.

Muktasari:

Faiza Salum, Mkuu wa Wilaya ya Itilima ndiyo mkuu wa wilaya pekee aliyeshinda katika nafasi hiyo mkoani humo, wakati Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura hakugombea nafasi yoyote ya uwakilishi ndani ya chama hicho.

Simiyu. Wakuu wa wilaya za Bariadi, Busega na Maswa mkoani Simiyu wameshindwa kupenya katika uchaguzi wa CCM wilaya katika nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu taifa ambapo mkuu wa wilaya ya Itilima, Faiza Salum akiibuka kidedea katika nafasi hiyo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Octoba 2, 2022, makamisaa hao wa CCM ngazi za wilaya, walikuwa wanawania nafasi ya uwakilishi wa wilaya katika mkutano mkuu wa taifa, nafasi yenye wajumbe watatu kutoka katika kila wilaya.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange ameshindwa kupenya katika nafasi hiyo iliyokuwa na wagombea 11 ambapo Kapange alishika nafasi ya saba akiwa na kura 196.

Wajumbe waliochaguliwa kuiwakilisha wilaya ya Bariadi ni Spora Nhwani aliyepata kura 495 akifuatiwa na Malongo Lukago aliyepata kura 444 na Seif Masoud Hamadi mwenye kura 366.

Wilaya ya Maswa ilikuwa na wagombea tisa huku mkuu wa wilaya hiyo, Aswege Kaminyoge akiambulia kura 416 akitanguliwa na George Lugomela aliyepata kura 1010, Pius Bunyongoli kura 850 na Jonathan Mnyela aliyepata kura 578.

Katika wilaya ya Busega, mkuu wa wilaya hiyo Gabriel Zakaria ameambulia kura 130 huku Feisal Ahmed akiongoza kwa kupata kura 577 akifuatiwa na Buluba Luteja mwenye kura 436 na  Dk Rafael Chegeni aliyepata kura 432.

Faiza Salum, mkuu wa wilaya ya Itilima ndiyo mkuu wa wilaya pekee aliyeshinda katika nafasi hiyo.  Mkuu wa wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura hakugombea nafasi yoyote ya uwakilishi ndani ya chama hicho.