Walalama kunyeshewa mvua, kusafiri na mifugo kwenye kivuko
Muktasari:
- Kisiwa cha Kome ni miongoni mwa visiwa 27 vilivyopo wilayani Sengerema ambacho asilimia 60 ya wakazi wa kisiwa hicho wanajihusha na uvuvi na asilimia 40 wanajihusisha na kilimo na shughuli nyingine za kujipatia kipato.
Buchosa. Kunyeshewa mvua, kubanana pamoja na kubeba abiria na mifugo kwa wakati mmoja ni miongoni mwa adha wanayokutana nayo wakazi wa Kisiwa cha Kome Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza katika Kivuko cha Kome II wanachokitumia.
Wananchi hao wamelalamikia kadhia hiyo kwa miaka kadhaa na ilipofika mwaka 2022, Serikali iliwaahidi kuwapelekea kivuko kipya cha Mv Kome III, ahadi ambayo haijakamilika ikiwa ni miaka mitatu sasa imepita tangu itolewe na Serikali.
Kivuko cha MV Kome II chenye uwezo wa kubeba tani 50 pekee, kinatoa huduma ya usafirishaji wa mizigo na abiria katika Ziwa Victoria kati ya Nyakaliro na Kome katika Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 6, 2024, mkazi wa kisiwa hicho, Amos John amesema licha ya kunyeshewa na mvua wakiwa ndani ya kivuko hicho, lakini pia ni kidogo hivyo huelemewa na abiria walioongezeka kisiwani humo kutokana na shuguli za kiuchumi.
Mkazi mwingine wa kisiwani hapo, Anastazia Julias ameiomba Serikali kuharakisha ahadi yake ya ujenzi wa kivuko cha Mv Kome III kwa kuwa wanachokitumia kinahatarisha maisha yao.
“Wakati wa masika abiria wanahangaika kivuko kinapokutana na upepo ziwani hupigwa wingi na kuleta wasiwasi kwa abiria wanaokuwa ndani ya chombo hicho,”amesema Hamis John, mkazi wa Kome
Ujenzi wa Mv Kome III
Msimamizi wa miradi kutoka Kampuni ya Songoro Marine, Isakwise Samwely amesema wakazi hao wataondokana na adha ya usafiri Februari, 2025 kivuko cha Mv Kome III kitakapokamilika na kuanza kutoa huduma.
“Kivuko hiki kwa sasa kimefikia asilimia 90 na kwa sasa tunapiga rangi, kuweka viti na tunaweka injini zake… kufika Februari, 2025 kitakuwa kimekabidhiwa kwa wananchi,” amesema Samwely.
Mkurugenzi Mtendaji wa Songoro Marine, Meja Songoro amesema ujenzi wa kivuko cha Mv Kome III kilitakiwa kukamilika Julai 31, 2023 lakini kimechelewa kutokana na changamoto iliyojitokeza nje ya uwezo wao.
Amesema kitakapokamilika kitabeba abiria 800, magari madogo 22 na kitakuwa na tani 170.
“Thamani tuliyopewa na Serikali nikubwa tutahakikisha tunakamilisha ujenzi wa vivuko hivi kwa wakati na kuzingatia thamani ya mradi husika,” amesema Songoro.
Meneja wa Vivuko kanda ya Magharibi, Vitalis Bilauri amewahakikishia wananchi wa Kome kuwa hadi kufikia Februari, 2025 kivuko cha Mv Kome III kitakuwa tayari kimekabidhiwa kwa wananchi na kuanza kutoa huduma.
Mmoja wa wakazi wa Kisiwa cha Kome, Yonas Mgabuzi aliyetembelea kivuko hicho kipya leo Jumatano, Novemba 6, 2024, amesema ni fahari kuona Serikali imesikia kilio chao cha muda mrefu na kuwa kitakapokamilika kitakuwa mkombozi kwao.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo amesema alikuwa ameweka rehani ubunge wake kama ahadi yake ya kupatikana kwa kivuko kipya isingetekelezeka.
“Wakazi wa Kisiwa cha Kome walikuwa na mateso kivuko walichokuwa wakitumia kwa sasa kimepitwa na wakati abiria wanachanganywa na wanyama hii ilikuwa inaleta adha kwa wananchi sasa mateso yanakwenda kuisha,” amesema Shigongo.