Walalamika kwa Mbowe tozo za sherehe, mazishi

Kigoma. Wakazi wa Muyama iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wameiomba Serikali kuingilia kati changamoto ya kutozwa Sh20,000 kwa ajili ya kupatiwa kibali cha kufanya mazishi.

Pia, wamesema halmashauri hiyo imepitisha tozo ya Sh20,000 kwa ajili ya kulipia kibali cha kufanya sherehe ya asili yenye lengo la kutoa zawadi kwa wanandoa na waliojifungua kwa jamii ya kabila la Waha maarufu kama "Kugemula".

Wananchi hao wametoa kilio hicho kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika jana katika uwanja wa Shule ya Msingi Nyanga wilayani Buhigwe.

"Manispaa imetafuta vyanzo vya mapato wakaona waweke kibali kwa ajili ya mazishi ambacho kinatolewa na Mwenyekiti wa Kijiji. Hivi mkazi wa kijijini huku amefiwa, halafu anatakiwa kulipia kibali cha kuzika mpendwa wake? Hii si sawa, tunaiomba Serikali iingilie kati," alisema Lameza Philipo.

Mkazi mwingine wa kijiji cha Muyama katika manispaa hiyo, Philomena Shija alisema, "Japo kuna utitiri wa ushuru katika manispaa yetu ikiwemo kutakiwa kulipia ushuru wa kufanya sherehe, kutozwa Sh1,750 kwa ajili ya kuweka heleni kwa kila ng'ombe, lakini hiyo ya kibali cha kuzika nimekuwa nikiisikia tu, sijawahi kufiwa hivi karibuni hivyo sielewi."

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Gaston Garubindi alisema utekelezaji wa maagizo hayo umeshaanza katika baadhi ya kata za manispaa hiyo huku akisema umekuwa kero kwa wakazi wanapofiwa.

"Ni ajabu kwamba sasa ukifiwa ukahitaji kwenda kuzika unatakiwa kulipa Sh20,000. Baadhi ya kata zimeanza kutekeleza kuna shida.

“Serikali inayosubiri misiba itokee ili wapate fedha hiyo haitaweza kutusaidia kuleta dawa kwa wananchi wake," alisema Garubindi

Hata hivyo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani humo, Essau Ngoloka alipopigiwa simu ili kuulizwa suala hilo iliita bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) haukujibiwa.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Tarafa ya Muyama, Eliya Michael bila kutaja idadi ya waliotozwa na sababu za uanzishwaji wake alipiga marufuku wenyeviti wa vijiji vya halmashauri hiyo kuwatoza wananchi fedha kwa ajili ya kuwapa kibali cha maziko.

Michael alikwenda mbali kwa kutishia kujiuzulu wadhfa wake endapo atabaini kuna mwananchi ametozwa Sh20,000 kwa ajili ya kulipia kibali cha mazishi kwa kile alichodai utaratibu huo unakiuka haki na mfumo wa maendeleo ya watu.

"Nimekuwa nikisikia tu kuwa baraza la madiwani lilipitisha utaratibu huo, lakini nitumie mkusanyiko huu kupiga marufuku tabia ya watendaji wa Serikali katika tarafa yangu kuwatoza wananchi fedha kwa ajili ya kutoa kubali cha mazishi," alisema Michael ambaye anasimamia kata saba za halmshauri hiyo.

Akihutubia katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu aliwataka wananchi kuchukulia changamoto ya utitiri wa tozo hizo kama sababu itakayowafanya washirikiane na Chadema kuiondoa CCM madarakani.

"Ni aibu kuona katika Halmshauri hii ambayo wanatokea viongozi wakubwa wa Serikali zinaanzishwa tozo ambazo ni mwiba kwa wananchi,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe aliwataka wananchi kutoishia kulalamika badala yake wawe mstari wa mbele kudai Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

Pia alisema chama hicho kinaamini katika misingi mikuu minne ambayo ni haki, uhuru, demokrasia na maendeleo ya watu, hivyo alisema uanzishwaji wa tozo hizo unakiuka misingi ya chama hicho.

"Haya madhaifu na changamoto zinazoonekana ni matokeo ya watunga sera kutoweka mbele maslahi ya umma na maendeleo ya watu, lakini kupitia Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi tutapata wawakilishi wa watu," alisema Mbowe.