Walemavu wataka kushirikishwa kutoa maoni utungaji sheria za nchi

Watu wenye ulemavu wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa mdahalo uliofanyika leo Kibaha Mkoa wa Pwani ukishirikisha na watoa maamuzi katika ngazi mbalimbali Serikalini,Wanasiasa na Viongozi wa Dini, Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Wenye Ulemavu waomba kupewa mikopo ya asilimia mbili na fursa ya kushirikishwa kwenye ngazi ya maamuzi.

Kibaha. Watu wenye ulemavu wa kusikia Mkoa wa Pwani wameiomba Serikali kuweka utaratibu utakaowawezesha kushirikishwa kwenye ngazi ya maamuzi juu na kutoa maoni ili kuondoa changamoto zinazowakabili pamoja na kunufaika na rasilimali za nchi.

Masuala ambayo wanadai kutoshirikishwa kwa ukamilifu na kusababisha kukosa fursa mbalimbali ni pamoja na kutoa maoni yao kwenye ngazi za maamuzi kabla sheria hazijapitishwa na kuanza kufanya kazi jambo ambalo limekuwa likisababisha wao kuwa nyuma kila wakati.

Wametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi Mosi, 2023 wakati wa mdahalo baina yao na watendaji wa ngazi mbalimbali serikalini, viongozi wa dini na wanasiasa uliofanyika Kibaha Mkoa wa Pwani.

Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Mkoa wa Pwani, Adamu Shabani amesema kuwa pamoja na mambo mengine ambayo wamekuwa wakikosa watu walio kwenye kundi hilo ni mikopo ya asilimia mbili kutoka halmashauri na kutoshirikishwa kwenye ngazi za maamuzi.

"Tumeandaa mdahalo huu leo kwa malengo mawili la kwanza ni kuelezea uhalisia juu ya watu wenye ulemavu hasa viziwi kutopata mikopo ya asilimia mbili kutoka halmashauri na pia kutoshirikishwa kwenye ngazi za maamuzi ikiwemo kwenye mabaraza ya madiwani," amesema.

Amesema kuwa anaamini kuwa baada ya mdahalo huo ulioshirikisha makundi mbalimbali, utaleta mabadiliko chanya kwa kundi hilo kukumbukwa na kunufaika na fursa hizo ambazo wamezikosa kwa muda mrefu.

"Tunashukuru kwa kupata ufadhiri kutoka Taasisi ya Foundation forĀ  Civil Society kwani tunaamini tutaleta mabadiliko kwa jamii pindi tutakapokamilisha mradi huu na kuwaletea matunda watu wenye ulemavu,"amesema.

Kwa upande wake, Thomasy Mponda amesema kuwa kwa miaka mingi watu wenye ulemavu wamekuwa hawashirikishwi kwa ukamilifu hata wakati wa kupitishwa kwa bajeti bungeni na badala yake inaoitishwa na watu wengine kwa niaba yao jambo ambalo ni kinyume.

Shehe wa Mkoa wa Pwani, Khamisi Mtupa amesema kuwa ni vyema watendaji wenye mamlaka mbalimbali wakatambua kuwa watu wenye ulemavu hawapaswi kupuuzwa kwakuwa wanaimani sawa na watu wengine.

"Zana iliyozoeleka kwa baadhi ya watu kudhani kuwa watu wenye ulemavu ni ombaomba inapaswa kupuuzwa kwakuwa inawadedhehesha na si kweli hali iko hivyo,"amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibaha, Josephin Gunda amesema kuwa wamekuwa wakiwashirikisha watu wenye ulemavu katika maamuzi mbalimbali kwani wanatambua kwamba wanahaki ya kufanyiwa hivyo.