Walimu elimu maalumu wahitajika Pwani

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Severa Salvatory akizungumza na Maafisa Elimu wa Halmashauri za mkoa huo kwenye kikoa cha kufanya tathmini ya maendeleo ya Elimu kilichofanyika Mjini Kibaha. Picha naSanjito Msafiri

Kibaha. Serikali imeombwa kuongeza ajira za walimu wa elimu maalumu nchini hali itakayowezesha wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali kupata fursa ya kijifunza masomo kwa ukamilifu kama ilivyo kwa watoto wengine.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Machi 22, 2023 Mjini Kibaha kwenye kikao cha maofisa elimu msingi na sekondari na wakuu wa shule kutoka Halmashauri za Mkoa wa Pwani kilichokuwa na lengo la kufanya tathmini ya maendeleo ya elimu kwa miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.

"Sisi Halmashauri ya Bagamoyo inahitaji walimu wa elimu maalumu 29 lakini waliopo ni 17 hivyo pungufu ni 12 jambo ambalo linawawia ugumu katika utekelezaji wa majukumu yao," amesema Wema Kajigili.

Kajigili ambaye ni Ofisa Elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Bagamoyo, amesema kuwa changamoto hiyo ni vyema ikafanyiwa kazi kwa wakati kwani walimu hao wana umuhimu hasa kukuza uelewa kwa wanafunzi wenye ulemavu ikiwemo uziwi.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Chalinze, Hamisi Shemahonge amesema kuwa uwiano wa walimu wa elimu maalumu hauendani na mahitaji jambo ambalo linawapa ugumu wanafunzi wenye uelemavu wakati wa kijifunza.

Awali, akifungua kikao hicho mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Severa Salvatory aliwataka watendaji hao kutekeleza majukumu yao kikamilifu  na kujiwekea malengo.

"Fanyeni vikao mara kwa mara kulingana na miongozo iliyopo ili kupata tathmini na mwenendo wa kazi na kama kuna changamoto mnazifanyia kazi kwa wakati," amesema.

Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani, Sara Mlaki  amewataka maafisa elimu pamoja na wakuu wa shule mkoani humo kuhakikisha wanaifanyia kazi changamoto ya kuondoa tatizo la baadhi ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika maarufu (KK)  ili kukuza kiwango cha elimu.

Amesema kuwa taarifa alizopata ni kwamba hali hiyo inachangia na wanafunzi wanaohamia kutoka mikoa mingine wanakuwa na tatizo hilo hivyo ni vema wakabainishwa ili kupata ufumbuzi wa kukabiliana nalo.