Walimu waliodaiwa kuvujisha mitihani waachiwa huru

Baadhi ya Walimu walioachiwa huru wakitoka nje ya ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora baada ya kuachiwa huru katika shauri la kudaiwa kuvujisha mitihani ya Hisabati na Kiswahili. Picha na Mpigapicha Wetu.

Muktasari:

Katika shauri hilo la jinai namba 49/2021, lililofunguliwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, walimu hao waliokuwa wakitetewa na Wakili, Kelvin Kayaga walidaiwa kuvujisha mitihani ya somo la Hisabati na Kiswahili wakati wa mitihani ya Taifa mwaka 2020.

Tabora. Walimu sita wa shule ya msingi Usagari Wilayani Uyui mkoani Tabora waliodaiwa kuvujisha mitihani ya Taifa ya darasa la saba wameachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa yao mahakamani.

Walimu hao ambao kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Oktoba 29, 2021, walikuwa wakikabiliwa na makosa saba ya kuvujisha mitihani ya somo la Hisabati na Kiswahili wakati wa mitihani ya Taifa ya darasa la saba mwaka 2020.

Shauri hilo la jinai namba 49/2021 lilikuwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora.

Katika hukumu yake ya April 24, 2023, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Sigwa Mzige amesema Mahakama hiyo inawaachia huru washtakiwa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa dhidi yao.

Katika kujenga kosa, upande wa mashtaka uliita mashahidi saba na kuwasilisha vielelezo kadhaa ikiwemo kishikwambi na makaratasi yaliyodaiwa kuwa na maandishi ya majibu ya mitihani ya somo la Kiswahili na Hisabati.

Wakijibu hoja za upande wa mashtaka kupitia kwa wakili wao, Kelvin Kayaga, washtakiwa waliibua hoja ya ukiukwaji wa sheria kuanzia ukamataji hadi kufikishwa mahakamani.

“Washtakiwa walikamatwa Oktoba  7, 2020 lakini ilichukua mwaka mzima hadi walipofikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yanayowakabili. Hii ni kinyume cha sheria inayoelekeza watuhumiwa kufikishwa mahakamani ndani ya Saa 24 tangu wanapokamatwa,” alidai wakili akiishawishi Mahakama kuwaachia huru wateja wake