Waliokuwa na magonjwa sugu walivyohudumiwa wakati wa corona

Waliokuwa na magonjwa sugu walivyohudumiwa wakati wa corona

Muktasari:

Kipindi cha corona staili ya maisha ilibadilika. Ndivyo unavyoweza kusema kwa kuwa ilikuwa nadra kushuhudia watu wakipeana mikono, kugusa uso, kuhudhuria sherehe na matukio muhimu na kutembelea sehemu mbalimbali.

Kipindi cha corona staili ya maisha ilibadilika. Ndivyo unavyoweza kusema kwa kuwa ilikuwa nadra kushuhudia watu wakipeana mikono, kugusa uso, kuhudhuria sherehe na matukio muhimu na kutembelea sehemu mbalimbali.

Tangu ugonjwa uliposhika kasi nchini na shughuli mbalimbali muhimu kusitishwa kwa muda wa takribani miezi miwili mambo kama hayo ndio yaliyozoeleka wakati huo.

Kila mmoja alifanya bidii kujilinda ili asipate maambukizi kwa kufuata taratibu zilizokuwa zimewekwa ikiwemo kuvaa barakoa, kunawa mikono.

Hata hivyo, kuna kundi lililokuwa kwenye hatari ya maambukizi ambalo ni watu waliokuwa sugu ikiwemo saratani, kifua kikuu, ukimwi na Lupus.

Wao walilazimika kujilinda mara mbili zaidi ya hali ya kawaida ili kuhakikisha kuwa wanavuka salama katika kipindi hiki.

“Wakati wa Covid-19 ilikuwa ni kikwazo kwetu kwani tulilazimika kukaa nyumbani muda mwingi ili kuepuka msongamano wa watu kwa sababu sisi ni miongoni mwa wale tunaoweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa haraka,” alisema Flora Mwinyimvua, mkazi wa Kimara.

Flora ambaye anatumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi, anasema uwepo wa ugonjwa huo ulibadili hata mfumo wa upataji dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi ‘ARVs’.

“Moja ya njia zilizotumika ilikuwa ni kuanzisha vituo vya dharura ambapo tulikuwa tunakwenda kuchukua dawa kwa watendaji kata.”

“Njia nyingine ilikuwa ni kutoa dawa za kudumu muda mrefu kwa miezi mitatu hadi sita kulingana na sehemu anayoishi mtu na hali yake alivyo,” alisema

Alisema baadhi pia walikuwa wanapelekewa huduma sehemu wanazoishi kwa kutumia gari maalumu ambapo mhusika alikuwa anapigiwa simu na kwenda kuchukua dawa.

“Namba za simu walizokuwa wanatumia ni kutoka kitabu cha wahudhuriaji wa Care Treatment Center (CTC) ambazo huonyesha tarehe ambayo mtu alichukua dawa na atachukua tena lini,” alisema.

Wakati Flora akieleza hayo,  Theresia John mkazi wa Kimara alibainisha kuwa walipokuwa wakipigiwa simu walielekezwa eneo ambalo gari litakuwa ili wachukue dawa na muda.

“Kwenye gari watu walikuwa wanaingia mmojammoja kuchukua dawa kiasi cha kufanya mtu yeyote aliye karibu asiweze kujua kinachoendelea humo ndani,” alisema Theresia.

Alisema jambo hilo lilikuwa likisaidia watu kupata dawa kwa wakati, kwani walikuwa wakipewa dawa siku moja kabla ya dozi ya zamani kuisha.

Alisema suala hilo liliwasaidia kuepuka msongamano na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma katika vituo vya afya, jambo ambalo lingeweza kusababisha wakapata maambukizi.

“Lakini kuna wale ambao maambukizi yao yako juu walikuwa wakilazimika kwenda kliniki kwa utaratibu ili kupatiwa vipimo na dawa.”

“Kwa sisi ambao tumeanza dawa muda mrefu na hatuna shida yoyote ilikuwa ni kuingia kusaini unapewa dawa na kuondoka,” anasema Theresia.

Corona  yawaathiri

Wakati mwingi wakitumia kukaa ndani ili kuhofia maambukizi, Flora anabainisha kuwa hali yake ya uchumi imedorora.

Hiyo ni kutokana na kulazimika kusimamisha shughuli zake za biashara alizokuwa akifanya ili kujilinda asipate maambukizi.

“Shughuli tena ndiyo zikasimama nikabaki kujilinda kwanza mwenyewe hadi pale hali itakapokuwa kawaida ndiyo nirejee,” alisema Flora ambaye pia ni mjasiriamali.

Wawili hao wanawakilisha kundi la watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na wanajua hali zao, vilevile wameingizwa katika mfumo wa matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU.

Lengo kuu la kutokomeza janga la Ukimwi ni kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao. Kutokana na takwimu kutoka Tanzania Health Portal ya mwaka wa 2019, 1,444,000 kati ya watu 1,600,000 wanaokadiriwa kuishi na VVU watalazimika kupimwa ili kufikia lengo la 90%. Hivi sasa, 86% ya watu wanaoishi na VVU nchini Tanzania wanajua hali yao.

Waliokuwa na magonjwa sugu walivyohudumiwa wakati wa corona

Vivyo hivyo, 90% ya watu wanaogundulika kuwa na VVU wanapaswa kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU ili kufikia lengo la kutokomeza janga la UKIMWI. Hivi sasa, asilimia 79.57% ya watu waliopatikana na VVU nchini Tanzania wanapokea dawa za kupunguza makali ya VVU.

Waliokuwa na magonjwa sugu walivyohudumiwa wakati wa corona

Katika hotuba ya Waziri mkuu Kassim Majaliwa katika maadhimisho ya siku ya ukimwi Desemba mosi,  2020 alibainisha kuwa vijana ni kundi linalokabiliwa na changamoto ya maambukizi mapya ya VVU nchini.

Takwimu za maambukizi mapya ya VVU zinaonesha kwamba asilimia 40 ya maambukizi hutokea kwa vijana na katika hao asilimia 80 ni wasichana.

Kwa mujibu wa takwimu hizo ni dhahiri kuwa kundi la vijana na hasa wa kike lipo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi mapya.

Lakini licha ya uwepo wa maambukizi hayo, kiwango cha watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kimepungua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2017.

Aidha, maambukizi mapya kwa mwaka nayo yamezidi kupungua kutoka watu 130,000 mwaka 2001 hadi 68,484 mwaka 2019. Pia, vifo vitokanavyo na Ukimwi kwa mwaka vimepungua kutoka vifo 85,000 mwaka 2001 hadi 21,529 mwaka 2019.

Licha ya uchukuaji wa dawa kutoka kwa watendaji wa kata kuonekana njia rahisi, iliibua unyanyasaji kwa jamii inayowazunguka wahusika hususani wale ambao walikuwa hawatambuliki.

“Jambo hili lilikuwa linaamsha msongo wa mawazo sana kwa wahusika kwa sababu watu walikuwa wanashangaa wanapomuona mtu akichukua dawa hizo na walikuwa hawajui kuwa ni mtu anayeishi na virusi vya ukimwi,” alisema.

Namna walivyowalinda

Dk Zainabu Mwinyimkuu kutoka Care and Treatment center (CTC) Chanika alisema wakati maambukizi ya corona yapo juu nchini walilazimika kutoa elimu kwa kina, kwa kuwa ni namna gani watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanapaswa kujilinda.

Kuwazuia kutoka nyumbani bila sababu za msingi, kwenda katika mikusanyiko ya watu ni moja ya njia walizokuwa wakishauriwa.

“Mbali na kubadilisha utoaji wa dawa pia kwa wale ambao walihitaji kuja vituoni tuliwawekea utaratibu maalumu kwa kuwagawa makundi ya kuja ili kuondoa msongamano,” alisema

Makundi hayo yaligawiwa kulingana na muda ambao mgonjwa itakuwa ni rahisi kwake kwenda. Wengine walipangiwa saa 4 hadi 6 asubuhi na wengine wakiingia kuanzia saa 6 mchana.

“Wakija kituoni walikaa kwa nafasi, kufuata alama katika mabenchi yao,” alisema Dk Zainabu.

Alisema uwepo wa corona haukushusha mahudhurio ya wagonjwa katika kliniki zao na badala yake walipatiwa huduma nje ya kituo.

“Kuna baadhi walikuwa wanaogopa kuja kupata huduma kwa kujinyanyapaa wenyewe unakuta mtu anatoa namba ya simu ya uongo ambayo ukimpigia haipatikani inakuwa ngumu kumpata,” alisema Dk Zainabu.

Dk Aafke Kinemo ambaye ni mratibu wa Fikia jijini Dar es Salaam ulio chini ya shirika la Icap Tanzania, alisema baada ya kuingia corona waliichukulia kama changamoto inayoweza kuzorotesha mahudhurio ya kliniki jambo ambalo lilifanya watafute ufumbuzi wa haraka.

“Tumekuwa tukiwapelekea wagonjwa wa virusi vya ukimwi dawa katika makazi yao tangu 2018, lakini baada ya Covid-19 tulitoa mapendekezo kwa mganga mkuu wa mkoa akayakubali na tukaanza huduma, kwa upande wa Ilala tulihudumia vituo 13 na Ubungo vituo 10.”

“Kupitia huduma hii zaidi ya watu 12,000 walifikiwa kati ya Aprili, Mei na Juni jambo ambalo liliwafanya wasipoteze uelekeo katika matumizi ya dawa zao,” alisema Dk Kinemo.

Huduma hii pia ilipatikana katika mikoa mingine ambayo baadhi ni Mwanza, Geita, Mara, Kigoma, Kagera na Pwani.

“Kupita huduma hii tulikuwa tunaendelea pia kutoa matibabu bila kusita na walifarijika,” alisema Kinemo.

Mkurugenzi wa kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Dk Leonard Subi alisema mpango wa utoaji dawa za kudumu muda mrefu kwa baadhi ya wagonjwa ulianza kutumika na utaendelea hata baada ya Covid-19 kumalizika.

Alisema dawa zilizokuwa zinatolewa ni za miezi mitatu kwa walio wengi huku akibainisha kuwa dawa za miezi 6 zilitolewa kwa wakazi wa Dar es Salaam pekee.

“Covid-19 ilipoingia kama nchi tuliandaa mwongozo wa namna bora ya kuhudumia wagonjwa wa VVU na bahati nzuri wagonjwa wetu wote walipata huduma vizuri na Covid-19 haikuwaathiri kwa sababu tulikuwa tunawapa dawa za muda mrefu.”

“Na hii haikuwa katika ukimwi tu, tulienda na magonjwa yote ikiwemo Kisukari, shinikizo za damu wote walikuwa wakipata dawa za muda mrefu na suala hili ni endelevu, halitakoma na ndivyo tunafanya kwa kufuata kanuni zilezile,” alisema Dk Subi.

Hivyo ni dhahiri kuwa endapo njia bora za kuhudumia watu walio na magonjwa sugu zitawekwa upo uwezekano wa wao kulindwa wasipate maambukizi ya magonjwa mengine kama ilivyokuwa kwa virusi vya corona.

Habari hii imeungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti Mgogoro.