Waliopata chanjo ya Uviko - 19 wafikia asilimia 34 ya lengo

Waliopata chanjo ya Uviko - 19 wafikia asilimia 34 ya lengo

Muktasari:

  • Wakati Watanzania waliochanjwa chanjo ya Uviko 19 wakifikia asilimia 34 ya lengo, Serikali inajiandaa kuzindua chanjo awamu ya pili ambayo inalenga kuwafikia watu wengi zaidi.

Dodoma. Serikali inajiandaa kuzindua chanjo ya Uviko-19 ambayo inatajwa kuwa inakwenda kugusa makundi ambayo hayakuwa yakifikika kwa urahisi.

Uzinduzi huo unatarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Oktoba ambapo utaratibu mzuri unawekwa kuonyesha namna gani wananchi watapata huduma hiyo.

Wakati huo taarifa ya Serikali imesema hadi sasa Watanzania waliochanjwa ni 345,000 ambayo ni asilimia 34 ya idadi ambayo Serikali ilipokea.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 12,2021 na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa mbalimbali za matukio ya Taifa katika utaratibu aliojiwekea.

Msigwa amesema hakuna kitu kigeni ukilinganisha na uzinduzi wa awali lakini lengo ni kufanya uhamasishaji wa wananchi na kuongeza vituo hadi Vijijini.

Amesema changamoto kubwa waliyobaini ni umbali wa mahali huduma zinakopatikana jambo linalokwamisha ufikaji wa wazee hivyo wanasogeza jirani.

Hata hivyo amesema Serikali inaendelea na uhamasishaji wa utoaji elimu kuhusu chanjo kutokana na faida zake kuwa kubwa hasa mtu anapopatwa na ugonjwa wa Uviko-19.