Walipa kodi wakubwa waonesha njia TRA kukusanya Sh11 trilioni
Muktasari:
Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/24 ni Sh44.39 trilioni huku TRA ikitarajiwa kukusanya mapato ya kodi ya Sh26.7 trilioni, kati ya hizo Sh11.98 trilioni sawa na asilimia 43 ya makusanyo ya TRA ikitarajiwa kukusanywa kutoka kwa walipa kodi wakubwa.
Mwanza. Ili kutimiza lengo la kukusanya mapato ya kodi ya Sh11.98 trilioni kutoka kwa walipa kodi wakubwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeshauriwa kudhibiti wafanyabiashara wanaofanya biashara kimagendo.
Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/24 ni Sh44.39 trilioni huku TRA ikitarajiwa kukusanya mapato ya kodi ya Sh26.7 trilioni, kati ya hizo Sh11.98 trilioni sawa na asilimia 43 ya makusanyo ya TRA ikitarajiwa kukusanywa kutoka kwa walipa kodi wakubwa.
Wakizungumza Agosti 21, 2023 mara baada ya kujengewa uwezo wa mabadiliko ya sheria ya fedha ya 2023/24 yaliyoambatana na semina ya mlipa kodi jijini Mwanza, walipa kodi wakubwa wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wamesema kudhibitiwa biashara za magendo kutaongeza mapato TRA.
“TRA wamesema wana target (lengo) ya kukusanya zaidi ya Sh11 trilioni kutoka kwetu walipa kodi wakubwa, nadhani wakijikita zaidi kwenye kupunguza biashara za magendo itawapa uwezo mkubwa wa kukusanya kodi kwa sababu watu watafanya biashara kihalali,”amesema Gladness Kileo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya East African Spirit mkoani Shinyanga
Amesema biashara za magendo haziwaathiri TRA pekee kwenye mapato, zinaathiri pia afya za wananchi na kuwarudisha nyuma walipa kodi wakubwa akidai wakiwa nyuma hata Serikali haiwezi kupata mapato; mwisho wa siku wanaofaidika ni wanaofanya magendo.
“Ni jambo la hamasa sisi kutufanya kuendelea kulipa kodi kwa sababu biashara za magendo ndo zinaturudisha nyuma sisi wafanyabiashara wakubwa na tukiwa nyuma ina maana Serikali tunaikwamisha kwenye masuala yake ya kodi na wanaofaidi ni wafanyabiashara wa magendo,”amesema
Mshauri wa kodi kutoka Kampuni ya Boart Longyear, Leah Turuka amesema TRA wakishirikiana na walipa kodi wakubwa kwa kuwaweka karibu pamoja na kusikiliza kero zao na kuzitatua watafanikisha lengo lao la kukusanya mapato kulingana na walivyopangiwa na Serikali.
Meneja Kodi wa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML), Godvictor Lyimo ameishauri mamlaka hiyo ya mapato kuendelea kutoa elimu akidai watu wengi wanaofanya biashara kwa magendo hawana elimu nzuri ya mlipa kodi kwa kufikiri wanaokoa sehemu ya kodi wanayopaswa kulipa badala yake wanajikuta wameingia kwenye gharama kubwa kutokana na faini watakazolipa baada ya kukamatwa.
“Tunaamini kutokana na elimu hii inayoendelea kutolewa na TRA walipa kodi wengi watapata ufahamu wa umuhimu wa kulipa kodi, umuhimu wa kupitisha bidhaa kwenye njia rasmi ili kuweza kulipa mapatao sahihi, kuokoa afya za walaji lakini pia kuisaidia Serikali kuongeza mapato,”amesema Lyimo
Akifungua mafunzo hayo, Kamishna wa walipa kodi wakubwa, Alfred Mregi amesema mafanikio ya kukusanya kiwango hicho cha kodi yanategemea michango ya walipa kodi wakubwa nakuwataka waendelee kuwasilisha ritani za kodi sahihi, kufanya malipo ya kodi sahihi na kwa wakati.
Akiongelea biashara za magendo amesema ni moja ya maeneo yanayosababishia Serikali kukosa mapato, kuhatarisha afya za watumiaji na usalama wa Taifa.
“Uingizaji wa bidhaa za magendo nchini hudumaza uzalishaji kwenye viwanda vya ndani na kuleta uwiano wa biashara usio sawa, Nawakumbusha wafanyabiashara, wamiliki wa vyombo vya usafiri na watu wanaoishi ukanda wa Ziwa Victoria na mipakani kwamba, uingizaji wa bidhaa nchini kwa magendo au bila kulipa kodi ni ukiukwaji wa sheria ya forodhani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004,”amesema
Amesema mzigo au mtu yoyote atakayekamatwa kuingiza kwa njia ya magendo pamoja na chombo kilichohusika kusafirisha mzigo huo vitataifishwa, akiwataka wananchi wanaoishi jirani na maeneo yenye bandari bubu kutojihusisha na biashara hiyo badala yake ishirikiane na TRA kuzuia, kupambana na kutoa taarifa za wakwepa kodi.